02. Hukumu zinazofungamana na maji

yameumbwa kuwa ni yenye kutwaharisha. Yanasafidha kutokana na uchafu na najisi. Kwa hiyo twahara haipatikani kwa kimiminika kingine kisichokuwa maji. Ikiwa maji yamefikia Qullatayn au ni yanayotiririka, hayawezi kunajisiwa na kitu chochote isipokuwa kile kinachobadilisha rangi yake, ladha yak au harufu yake. Yasipokuwa hivyo, maji yanakuwa najisi kwa kuchanganyika na najisi. Qullatayn ni kiasi kinachokaribia takriban lita 300.

Ikiwa kitu ambacho si twahara kimepikwa ndani ya maji, ikiwa maji yatachanganyika na kitu kingine ambacho kikafanya kupoteza jina lake au maji yakatumika kuondoa uchafu, basi maji hayo hupoteza sifa yake ya kutwaharisha.

Ikiwa mtu ana shaka kuhusu usafi wa maji au kitu kingine, au kuhusu unajisi wake, basi msingi ni hali ya yakini. Ikiwa sehemu ya najisi imefichikana katika nguo au kitu kingine, basi ataosha sehemu anayoyakinisha kwamba najisi ipo. Na ikiwa maji ya kutwaharisha yatachanganyika na maji najisi na asipate maji mengine, basi atafanya Tayammum na kuyaacha yote mawili. Na ikiwa maji ya kutwaharisha yatachanganyika na maji yaliyo safi, basi atatawadha kwa kutumia kila moja kati ya hayo mawili. Na ikiwa nguo safi zitachanganyika na nguo najisi, ataswali katika kila nguo kwa idadi ya nguo najisi, kisha ataongeza swalah moja.

Najisi ya mbwa na nguruwe huoshwa mara saba, mojawapo ikiwa kwa udongo. Katika najisi nyingine yote inatosheleza kuosha mara tatu zinazoondoa najisi. Ikiwa najisi iko ardhini, kumimina maji mara moja yanayoondoa kiini chake kunatosheleza. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Miminieni juu ya mkojo wa bedui ndoo ya maji.”[1]

Katika mkojo wa mtoto wa kiume ambaye hajaanza kula chakula, kumwagia maji kunatosheleza. Vivyo hivyo hukumu hiyohiyo inatumika juu ya madhiy. Husamehewa kiasi chake kidogo – kiasi ambacho hakichukizi sana nafsi – pamoja na damu kidogo na kile kinachotokana nayo, kama vile usaha na mafinyo na mfano wake. Manii ya mwanadamu na mkojo wa mnyama ambaye nyama yake huliwa ni twahara.

[1] al-Bukhaariy (219) na Muslim (284).

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 13
  • Imechapishwa: 30/09/2026