02. Hadiyth ya Thawbaan kuhusu kupangusa juu ya soksi ni Swahiyh

1 – Ama Hadiyth ya Thawbaan, ameipokea Imaam Ahmad (5/277) kupitia kwa Yahyaa bin Sa‘iyd, kutoka kwa Thawr, kutoka kwa Raashid bin Sa‘d, kutoka kwa Thawbaan. Vivyo hivyo ameipokea Abu Daawuud kupitia kwa Imaam Ahmad bin Hanbal kwa cheni hii ya wapokezi. Pia ameipokea al-Haakim katika ”al-Mustadrak (1/169) kupitia njia ya Imaam Ahmad, ambaye ameisahihisha kwa masharti ya Muslim na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

Thawr anaitwa bin Yaziyd al-Kalaa‘iy al-Himswiy. Alikuwa ni madhubuti na anayetambulika.

Raashid bin Sa‘d al-Himswiy naye pia alikuwa ni madhubuti. al-Bukhaariy amemtaja katika ”at-Taariykh al-Kabiyr” (2/1/266–267) bila kumtaja kwa jeruhi yoyote. Ina maana kwamba alikuwa anaonelea kuwa ni madhabuti. Ibn Abiy Haatim amemtaja katika ”al-Jarh wat-Ta‘diyl” (1/2/483) akanukuu namna ambavyo Yahyaa bin Ma‘iyn na Abu Haatim walikuwa wakionelea kuwa ni mtu madhubuti.

Ama kuhusu Imaam Ahmad kuitia kasoro Hadiyth hii kwa kukatika kwa cheni kati ya Raashid na Thawbaan. Mfano wa kauli hiyo imenukuliwa na Ibn Abiy Haatim katika ”al-Maraasiyl”, uk. 22, Ibn Abiy Haatim amepokea kutoka kwa ´Abdullaah bin Ahamd bin Hanbal, ambaye ameeleza ya kwamba baba yake amesema:

”Raashid bin Sa‘d hakumsikia Thawbaan.”

Lakini hili linapingwa na kauli ya al-Bukhaariy aliyekata kauli katika ”at-Taariykh al-Kabiyr” kuwa alimsikia. Amesema:

”Alimsikia Thawbaan na Ya‘laa bin Murrah.”

Haya yanatosha kuwa hoja katika kuthibitisha kumsikia kwake Thawbaan. Kwa hivyo hapana tena haja ya lile alilojitwisha mtunzi (Rahimahu Allaah) katika kupendelea kujengea hoja juu ya riwaya zenye kukatika. Kwa sababu chenye nguvu zaidi kwa wanazuoni wengi wa Hadiyth ni kwamba Hadiyth yenye kukatika huwa ni Hadiyth dhaifu na isiyofaa kujengewa hoja. Ama Hadiyth hii, imebainika kuwa ni Hadiyth iliyoungana na Swahiyh kwa cheni ya wapokezi.

  • Muhusika: ´Allaamah Ahmad Shaakir (afk. 1377)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 4-6
  • Imechapishwa: 31/03/2026