Sahl bin Muzaahim amesema:

”Hali ya mwanachuoni ni ngumu zaidi kuliko kufungwa mkono. Ni sahihi kwamba mjinga hapewi udhuru kutokana na ujinga wake, lakini mwanachuoni anaadhibiwa kwa ukali zaidi akiacha kutendea kazi elimu yake kwa vitendo.”

Ni kipi kilichowafanya Salaf kuwa na ngazi za juu kama sio kwa ajili ya imani zao safi, matendo mema na kutozama zaidi katika starehe za maisha ya dunia? Ni kipi kilichowafanya watu wenye hekima kufikia furaha ya juu zaidi kama sio kwa kufanya kazi kwa nguvu, kuridhika na yaliyo mepesi na kujitolea kile chenye kuzidi kumpa mwombaji na yule mwenye kunyimwa? Je, mkusanya vitabu si kama mkusanya fedha na mchimba dhahabu? Je, mwenye kuyafanyia ubakhili si kama mwenye kuvifanyia ubakhili viwili hivyo? Je, haadhibiwi yule mwenye kuvipenda kama ambaye anavilimbikiza viwili hivyo? Kama ambavo pesa hazinufaishi isipokuwa kwa kuzitoa, basi vivyo hivyo elimu hainufaishi isipokuwa kwa yule mwenye kuitendea kazi kwa vitendo na akayachunga majukumu yake.  Kwa ajili hiyo kila mmoja aiangalie vyema nafsi yake na achunge vizuri wakati wake. Kwani maisha ni mafupi, kifo kiko karibu, njia ni yenye kutisha, ughurikaji ndio kumeshinda, khatari ni kubwa, mkosoaji ni mwenye uoni wa ndani, Allaah (Ta´ala) ni Mwenye kuchunga na kila kitu ni chenye kurejea Kwake:

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri sawa na uzito wa chembe ya atomu, basi ataiona, na yule atakayetenda shari sawa na uzito wa chembe ya atomu, basi ataiona.”[1]

1 – al-Qaadhwiy Abu Bakr Ahmad bin al-Hasan bin Ahmad al-Harashiy ametukhabarisha: Abul-´Abbaas Muhammad bin Ya´quub al-Aswamm ametuhadithia: Muhammad bin Ishaaq as-Swaghaaniy ametuhadithia: al-Aswad bin ´Aamir ametukhabarisha: Abu Bakr bin ´Ayyaash ametukhabarisha: kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Sa´iyd bin ´Abdillaah, kutoka kwa Abu Barzah al-Aslamiy (Radhiya Allaahu ´anh), aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Haitovuka miguu ya mja siku ya Qiyaamah mpaka aulizwe juu ya mambo manne: umri wake aliuteketeza katika mambo gani, elimu yake aliifanyisha nini, mali yake aliipata kivipi na akaitumia wapi na mwili wake aliutumia vipi.”[2]

[1] 99:07-08

[2] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Ameipokea ad-Daarimiy na at-Tirmidhiy, ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr Ahmad bin ´Aliy al-Khatwiyb al-Baghdaadiy (afk. 463)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Iqtidhwaa’-ul-´Ilm al-´Amal, uk. 15-17
  • Imechapishwa: 06/05/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy