01. Utangulizi wa Ahmad Shaakir wa ”al-Mash ´alaal-Jawrabayn”

Sifa njema zote ni za Allaah Mola wa walimwengu wote, sifa nyingi zilizojaa baraka kama Anavyopenda Mola wetu na Anavyoridhika. Swalah na salamu zimshukie mbora wa Manabii na Mitume, mwisho wa Manabii na kiongozi wa wanadamu, bwana wetu Muhammad, pamoja na jamaa zake na Maswahaba wake wote.

Hakika mwalimu wetu, mwanazuoni wa Shaam, Shaykh Muhammad Jamaalud-Diyn al-Qaasimiy (Rahimahu Allaah) aliandika kijitabu chenye thamani kubwa kuhusu kupaka juu ya soksi. Kilichapishwa Dameski mwaka 1332. Nilikisoma na nikafaidika nacho elimu nyingi sana na nguvu ya kimaadili katika zama zile za mbali tulipokuwa mwanzoni mwa ujana hali ya kuwa na shauku kubwa ya kupata elimu sahihi – elimu ya Qur-aan na Sunnah. Tulikuwa na hamu kubwa sana ya vitabu vya Salaf na vitabu vya wale waliotembea juu ya mwenendo wao miongoni mwa waliokuja baadaye ambao wanashikamana na uongofu wa kinabii na wanaofuata dalili sahihi bila kasumba za maoni au matamanio na bila ufuataji kichwa mchunga.  Miongoni mwa waliokuwa mstari wa mbele kutembea juu ya mwenendo ulionyooka alikuwa mwalimu wetu al-Qaasimiy (Rahimahu Allaah). Alitembelea Misri kabla ya kufariki kwake na nilikuwa miongoni mwa wanafunzi waliowasiliana naye, wakahudhuria kwake na kufaidika kutokana na mwelekeo wake kuelekea njia iliyonyooka na mwenendo ulio sawa.

Rafiki yetu mpendwa, Salafiy mkubwa, mheshimiwa na mtukufu, ndugu yetu Muhammad Nasiyf alipenda kijitabu hiki kichapishwe tena baada ya kuwa adimu kupatikana na shauku ya watu kuimiliki ikaongezeka kwa lengo la kueneza manufaa yake. Akanitaka niisome tena na niandike utangulizi wake. Nikamweleza kuwa nina hamu ya kuhakiki baadhi ya Hadiyth alizozitumia kama dalili mtunzi (Rahimahu Allaah na kuongeza dalili nyingine zinazounga mkono yale aliyoona ambazo hazikuwa mbele yake alipoiandika kijitabu chake.

Dalili za msingi ambazo mtunzi wa kitabu amezijengea kitabu chake ni Hadiyth tatu. Hadiyth ya kwanza ni ya Thawbaan, Hadiyth ya al-Mughiyrah bin Shu´bah na Hadiyth ya Abu Muusa al-Ash´ariy. Basi nikaandika maneno haya nikibainisha dalili za usahihi wa Hadiyth hizi tatu. Nikaongeza juu yake dalili ya nne; nayo ni Hadiyth ya Anas bin Maalik. Nimejitahidi katika niliyoyaandika kadiri nilivyoweza. Ninamuomba Allaah anipe tawfiyq, msaada na usahihi. Hakika Yeye ni Msikivu wa maombi.

  • Muhusika: ´Allaamah Ahmad Shaakir (afk. 1377)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 3-4
  • Imechapishwa: 31/03/2026