45. Maovu ya tano: Kunyoa ndevu

05- Kunyoa ndevu

Jambo la tano: Ada nyingine mbaya – au pengine ikawa ni mbaya zaidi kwa wale wenye maumbile yaliyosalimika – ni yale waliyopewa mtihani kwayo wanaume wengi ambapo wanajipamba kwa kunyoa ndevu kwa sababu ya kuwafuata kichwa mchunga wazungu makafiri kiasi cha kwamba wanaona ni jambo la aibu bwanaharusi kuingia kwa bibiharusi hali ya kuwa na ndevu[1]. Katika hali kuna mikhalafa mingi ikiwa ni pamoja

1- Kubadilisha maumbile ya Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu shaytwaan:

لَّعَنَهُ اللَّـهُ ۘ وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنْ عِبَادِكَ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللَّـهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا

“Allaah amemlaani na akasema: “Hakika nitashika katika waja Wako sehemu maalum na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio na nitawaamrisha. Basi watakata masikio ya wanyama na nitawaamrisha watabadili maumbile ya Allaah. Na yule atakayemfanya shaytwaan kuwa rafiki badala ya Allaah, basi hakika amekhasirika khasara ya wazi kabisa.”[2]

Hii ni dalili ya wazi kabisa ya kwamba kubadilisha maumbile ya Allaah pasi na idhini kutoka Kwake (Ta´ala) ni kutii amri ya shaytwaan na kumuasi Allaah (Jalla Jallaaluh). Hapana shaka ya kwamba laana ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa wale wanawake wanaobadilisha maumbile ya Allaah kwa ajili ya kutafuta uzuri – kama ilivyotangulia nyuma – inawahusu vilevile wale wanaume wanaonyoa ndevu zao kwa ajili ya kutafuta uzuri. Khaswa ukizingati ya kwamba mawili hayo yanashirikiana katika sababu, kama ambavyo iko wazi. Nimesema “… pasi na idhini kutoka kwa Allaah (Ta´ala)” ili mtu asije kufikiria kwamba kunyoa nywele za sehemu za siri na nyenginezo ambazo Shari´ah imeruhusu kunaingia katika kubadilisha maumbile yaliyotajwa. Mambo hayo aidha yamependekezwa au yamewajibishwa.

2- Kwenda kinyume na amri yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

“Punguzeni masharubu na ziacheni ndevu.”[3]

Ni jambo linalotambulika ya kwamba maamrisho yanafidisha uwajibu isipokuwa kukiwepo dalili. Dalili hapa inatilia nguvu juu ya uwajibu. Nazo ni zifuatazo:

3- Kujifananisha na makafiri. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Punguzeni masharubu na ziacheni ndevu, jitofautisheni na majusi.”[4]

4- Kujifananisha na wanawake. Hakika “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamke mwenye kujifananisha na wanaume na mwanaume mwenye kujifananisha na wanawake.”[5]

[1] Kuna wengine wamepindukia katika upotevu na wamefanya kufuga ndevu ni katika mnasaba wa kufiwa na ndugu:

فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ

“Hakika hayapofuki macho, bali zinazopofuka ni nyoyo ziliomo vifuani.” (22:46)

[2] 04:118-119

[3] Ameipokea al-Bukhaariy (01/289) na matamshi ni yake, Muslim (01/153), Abu ´Awaanah (01/189) na wengineo kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhum).

[4] Muslim, Abu ´Awaanah katika “as-Swahiyh” zao kupitia kwa Abu Hurayrah.

[5] Ameipokea al-Bukhaariy (10/274), at-Tirmidhiy (02(129) na wengineo.

Miongoni mwa mambo yasiyokuwa na shaka kwa wale ambao maumbile yao yamesalimika ni kwamba kila dalili katika dalili hizi nne zinatosha juu ya kuthibitisha uwajibu wa kufuga ndevu na uharamu wa kuzinyoa. Tusemeje zikikusanyika zote nne? Kwa ajili hiyo Shaykh-ul-Islaam amesema:

“Imeharamishwa kunyoa ndevu.”

Hivyo ndivyo ilivyotajwa katika “al-Kawaakib ad-Daraariy” (02/101/01).

Nimezungumza kwa urefu kidogo juu ya masuala haya katika makala ambayo gazeti la “ash-Shihaab” walilieneza katika idadi ya (41) katika mwaka wa kwanza. Kisha baadhi ya wapenzi wa Sunnah na wale wanaopambana katika njia yake wakalieneza katika kijitabu kizuri kwa ajili ya kukichapisha na kukieneza huko Baghdaad. Ndani yake nimetaja dalili za wanachuoni juu ya uharamu wa kuzinyoa tukinukuu kuanzia kwa wale maimamu wanne. Yule anayetaka kukisoma basi arejee huko.

Ndugu! Usidanganyike na wale wengi waliopewa mtihani wa kwenda kinyume na jambo hili ijapokuwa katika wao kutakuwa baadhi ambao wanajinasibisha na elimu. Hakika yule mjinga ambaye anatendea kazi ile miongozo na nuru iliyokuja kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mbora kuliko [huyo mwanachuoni] na khaswa ikiwa atatumia elimu hii katika kuyapindisha maandiko yaliyo wazi na kuyatupilia mbali kwa sababu ya kufuata matamanio na ujasiri kama wanavosema baadhi yao:

“Hakika kufuga ndevu sio katika mambo ya dini. Bali ni katika mambo ya dunia ambayo muislamu amepewa khiyari.”

Wanasema hivi pamoja na kuwa wanatambua ya kwamba kufuga ndevu ni katika maumbile, kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokana na yale aliyopokea Muslim na wengineo. Isitoshe maumbile hayakubali kubadilisha Shari´ah. Amesema (´Azza wa Jall):

فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚ لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

“Umbile la asili la kumpwekesha Allaah ambalo kawaumba watu kwalo; hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah – hivo ndio dini iliyonyooka kisawasawa, lakini watu wengi hawajui!” (30:30)

Ee Allaah! Tuthibitishe kwa neno thabiti katika maisha ya dunia na Aakhirah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 207-212
  • Imechapishwa: 29/04/2018