Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Lau Allaah asingeliteremsha hoja yoyote kwa viumbe Wake isipokuwa Suurah hii, basi ingeliwatosheleza.”

al-Bukhaariy amesema:

“Mlango: Elimu kabla ya kauli na kitendo. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

“Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.” (Muhammad 47 : 19)

Akawa ameanza kwa elimu kabla ya kauli na kitendo.”

MAELEZO

ash-Shaafi´iy Alikuwa ni Abu ´Abdillaah Muhammad bin Idriys bin al-´Abbaas bin ´Uthmaan bin Shaafiy´ al-Haashimiy al-Qurayshiy. Alizaliwa Ghazzah mwaka wa 150 na alifariki Misri mwaka 204. Ni mmoja katika wale maimamu wane – rehema za Allaah (Ta´ala) ziwe juu yao wote!

Makusudio yake (Rahimahu Allaha) ni kwamba Suurah hii ni yenye kumtosheleza kiumbe kwa kumhimiza katika kushikamana barabara na dini kwa imani, matendo mema, kulingania katika dini ya Allaah na kuwa na subira juu ya hilo. Anachokusudia si kwamba Suurah hii inawatosheleza viumbe katika Shari´ah yote.

Mtu mwenye busara na uoni wa mbali pindi anaposikia au kuisoma Suurah hii basi ni lazima akimbilie kujikwamua na khasara hii. Hili linapitika kwa yeye kusifika na sifa hizi nne; imani, matendo mema, kuusiana kwa haki na kuusiana kwa subira.

al-Bukhaariy Alikuwa ni Abu ´Abdillaah Muhammad bin Ismaa´iyl bin Ibraahiym bin al-Mughiyrah al-Bukhaariy. Alizaliwa Bukhaaraa katika mwezi wa Shawwaal mwaka wa 194 na alikulia akiwa ni yatima chini ya ulezi wa mama yake. Alifariki (Rahimahu Allaah) katika usiku wa kuamkia ´Iyd-ul-Fitwr mwaka wa 256 Khartank mji ambao uko maili mbili tatu kutoka Samarkand.

al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) ametumia dalili kwa Aayah hii juu ya kuonyesha kwamba ni lazima kuanza kwa elimu kabla ya kauli na kitendo. Dalili hii ya mapokezi inafahamisha kwamba mtu anatakiwa kwanza kujifunza baada ya hapo ndio atende. Vilevile kuna dalili za kiakili zinazojulisha kuwa elimu inakuja kabla ya kauli na kitendo. Hilo ni kwa sababu kauli au kitendo hakiwezi kuwa sahihi na chenye kukubalika isipokuwa mpaka kiwe kimeafikiana na Shari´ah. Wakati huohuo mtu hawezi kujua ya kwamba kitendo chake kimeafikiana na Shari´ah pasi na elimu. Hata hivyo kuna mambo ambayo mtu anayajua kwa maumbile yake. Mfano wa elimu hiyo ni kama mtu kujua ya kwamba Allaah ndiye Mungu wa haki mmoja. Maumbile haya mja ameumbwa kwayo na kwa hivyo mtu hahitajii kutilia umuhimu mkubwa katika kuyasoma. Ama mambo ya sehemusehemu yaliyoenea ndio ambayo yanahitajia kuyasoma na kutumia juhudi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 26-28
  • Imechapishwa: 17/05/2020