03. Uhudhuriaji wa wanawake wenye hedhi unazidi kutilia nguvu ni wapi panaposwaliwa ´iyd

Kisha wakasema:

“… kwa sababu ya haja ya kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio maana aliswali msikitini kwa sababu ya udhuru.”

Halafu wakaiwekea taaliki Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) juu ya swalah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) msikitini kwa sababu ya udhuru uliozuka wa mvua.

Hata Hadiyth ya Abu Hurayrah lau ikiwa kama imesihi, bado ni hoja yetu. Hata yenyewe kinachopata kufahamika ni kuwa lau isingelikuwa sio kwa sababu ya udhuru wa mvua angeliswali uwanjani. Hakuna waislamu wanaoenda kinyume na hili isipokuwa nyinyi peke yenu. Maneno yenu yaliyotangulia yanaashiria kuwa kuswali sehemu ya uwanja ni jambo halikuwekwa katika Shari´ah hii leo kwa sababu mnaonelea kuwa ni jambo lisilowezekana. Pamoja na hivyo tumewaraddi kwa Hadiyth ikawa ni hoja dhidi yenu na si hoja yenye kuwasapoti – na yote haya ni endapo Hadiyth yenyewe itakuwa ni Swahiyh. Uhakika wa mambo ni kuwa sio Swahiyh. Mlolongo wa wapokezi wake ni dhaifu, jambo ambalo tutalibainisha huko mbeleni.

Maneno yao mengine yasiyokuwa na maana hayastahiki kujibiwa. Isipokuwa tu maneno yao baada ya kunukuu Hadiyth ya kwanza yenye kutoka kwenye Hadiyth ya Abu Sa´iyd inayokuja na Abu Hurayrah:

“Faida tunayopata ni kwamba inasihi kuswali sehemu ya uwanja na pia msikitini na yote mawili kunapatikana thawabu ndani yake. Faida nyingine tunayopata katika Hadiyth ya kwanza ni kuwa lililo bora zaidi ni kuswali nje jangwani kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku zote alikuwa akilazimiana na hilo.”

Ndugu msomaji! Tazama jinsi wanavyorudi katika haki ambayo sisi tunalingania kwayo! Kwa hayo wanayavunja maneno yao ya hapo kabla pamoja na sisi. Lakini hivi kweli unafikiria kuwa watabaki kuwa hivyo? Hapana! Hatimaye wamerudi kule walikoanzia na wakasema baada ya kunukuu maneno yafuatayo ya Imaam ash-Shaafi´iy yaliyonukuliwa na Haafidhw Ibn Hajar:

“Yule mwenye kutupia jicho Hadiyth ya al-Bukhaariy[1] iliyotangulia kutoka kwa Umm ´Atwiyyah:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuamrisha kuwatoa katika [´Iyd] al-Fitwr na [´Iyd] al-Adhwhaa´; wanawali,  wenye hedhi na wasichana mabikira. Ama wale wenye hedhi watajitenga na swalah.” Katika upokezi mwingine imekuja: “… uwanja wa kuswalia na watashuhudia kheri na ulinganizi wa waislamu.”[2]

anapata kutambua kuwa sababu iliyopelekea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kulazimiana siku zote kuswali sehemu ya uwanja ni ima msikiti wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukuwepo nafasi ya wanaume na wanawake kwa siku mbili, au msikitini sio sehemu inayofaa kwa wanawake wenye hedhi.”

Tumeyazingatia maneno yote haya na kuona kuwa hayana maana ni kama maneno yao mengine. Lau tutakubaliana nao kuwa msikiti wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakukuwepo nafasi yenye kuwatosha wanaume na wanawake wote, basi inatakiwa kutambulika kuwa hali kadhalika misikiti yetu hii leo. Hakuna msikiti hata mmoja ulio na nafasi ya kuwatosha waswaliji wote na hapo itabaki kuwa ni jambo limewekwa katika Shari´ah kutoka kwenda kuswali sehemu ya uwanja, jambo ambalo ndilo linalotakikana. Jengine ni kuwa ikiwa wao wanaonelea kuwa misikiti haifai kwa wanawake wenye hedhi kuhudhuria, basi ni lazima wakubali kuwa sehemu ya uwanja panawafaa. Wakilazimiana na kuswali misikitini, basi wamewakosesha kushuhudia mema na du´aa ya waislamu. Hili linaenda kinyume na kitendo cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ambayo wao wanaiegemeza kwa al-Bukhaariy. Hadiyth ni moja katika dalili zetu zinazojulisha kuwa swalah inatakiwa iwe sehemu ya uwanja na sio msikitini. Pasi na kujali namna msikiti ulivyo mkubwa, ni jambo lisilowezekana kwa wanaume na wanawake wote wakapata nafasi ndani yake, jambo ambalo wao wamenyewe wamelikiri.

Moja miongoni mwa hoja zetu kwao ni pale waliposema:

“Wanawake, mpaka wenye hedhi, walikuwa wakitoka kwenda uwanjani na wakileta Takbiyr pamoja na Takbiyr zao.”

Ni vipi mnaweza kuhakikisha Sunnah hii misikitini? Hamna njia ya kufanya hivo isipokuwa ikiwa kama mtawazuia kuhudhuria kabisa kabisa, jambo ambalo linaenda kinyume na kitendo chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo mnaweza kuwaamrisha kutoka na kubaki nje ya msikiti. Lakini vipi wataleta Takbiyr pamoja na waislamu wengine? Ndugu msomaji muislamu! Tazama namna ujinga unavyowafanya wenye nao na pata mazingatio!

[1] Ni kosa kumwegemezea Hadiyth hii al-Bukhaariy; ameipokea Muslim (3/20-21).

[2] al-Bukhaariy, Muslim na wengineo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 8-11
  • Imechapishwa: 12/05/2020