Swali: Tumesikia kutoka kwa baadhi ya ndugu kwamba nyinyi mmekataa Hadiyth ya Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwa njia tano. Tunaomba mtubainishie hizo njia tano?

Jibu: Ndiyo, ameipokea Abu Daawuud kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwamba Asmaa´ bint Abiy Bakr – ambaye ni dada yake mkubwa wa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) – aliingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa na nguo nyepesi, basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamgeukia mbali na akasema:

“Ee Asmaa´! Hakika mwanamke anapofikia hedhi basi haifai kuonekana kutoka kwake isipokuwa hii na hii” ambapo akaashiria uso wake na viganja vyake.”

Baadhi ya watu wamejengea hoja Hadiyth hii kuwa ni dalili ya kujuzu kufunua mwanamke uso wake na mikono yake na wakasema kwamba Hadiyth hii ya Asmaa´ inajulisha hivo, kwamba uso si uchi na kwamba hakuna kizuizi kwa mwanamke kujifunua mbele ya wanaume na wamejishikamanisha na Hadiyth hii. Wanazuoni wameijibu kwamba ni dhaifu na haisihi kujishikamanisha nayo na wala haisihi kuitumia kama hoja. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim ambao wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema maneno yenye maana kwamba walikuwa kabla ya Hijaab wakifunua nyuso zao. Basi iliposhuka Hijaab walifunika nyuso zao. Hilo lilikuwa katika vita vya Ifk, alipomsikia Swafwaan bin al-Mu‘atwwal akisema “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika Kwake tutarejea”. Niliposikia sauti yake nilifunika uso wangu na alikuwa ameniona kabla ya Hijaab. Anaashiria maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ

”Mnapowauliza haja, basi waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.”[1]

Baadhi ya wanazuoni wa Hadiyth wamesema kwamba Hadiyth ya Asmaa´ inaonyesha kinyume na Hadiyth ya ´Aaishah hii iliyo ndani ya al-Bukhaariy na Muslim na kwamba inaonyesha kujuzu kufunua uso na mikono. Wamejibiwa kwa majibu kadhaa. Nilitaja matatu katika masuala ya kuhusu Hijaab, kisha katika “Nuur ´alaad-Darb” nikataja nyongeza ya njia mbili ambapo zikawa zote tano. Zote zinaonyesha kutosihi kwa Hadiyth hii:

1 – Hakika mpokezi kutoka kwa ´Aaishah, ambaye anaitwa Khaalid bin Durayk, hakukutana na ´Aaishah. Kwa hiyo ni Hadiyth yenye kukatika. Hadiyth iliyokatika haitumiki kama hoja kwa udhaifu wake, kwa sababu hakukutana naye. Upokezi wake kutoka kwake umekatika.

2 – Katika cheni ya wapokezi kuna mtu anayeitwa Sa‘iyd bin Bashiyr, naye ni dhaifu. Hakutumiwi kama hoja upokezi wake.

3 – Hakika Qataadah aliyepokea kutoka kwa Khaalid amepokea kwa mfumo wa kutotaja kusikia moja kwa moja. Naye ni mwenye kufanya hadaa. Anapokea kutoka kwa wasiojulikana na mfano wao na anaficha hilo. Ikiwa hatataja kusikia, basi upokezi wake unakuwa dhaifu.

4 – Hakika Hadiyth haina uwazi kwamba hili lilikuwa baada ya Hijaab. Inawezekana lilikuwa kabla ya kufaradhishwa Hijaab. Kwa hiyo ´Aaishah hakusema kwamba kuingia kwake kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kulikuwa baada ya kufaradhishwa Hijaab. Hivyo basi inawezekana lilikuwa kabla ya kufarahishwa Hijaab.

5 – Hakika Asmaa´ ni mke wa az-Zubayr bin al-‘Awwaam, ni dada yake ´Aaishah bint as-Swiddiyq ambaye ni mwanamke katika bora wa wanawake kwa dini na akili. Basi inawezekanaje kwake kuingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – ambaye ni mwanamke mwema – akiwa na nguo nyepesi akifunua uso na mikono. Zaidi ya hayo akiwa na nguo nyepesi ambazo zinaonekana viungo visivyotakiwa kuonekana? Halidhaniwi hili kwa Asmaa´ (Radhiya Allaahu ´anhaa). Haidhaniwi kwake kuingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika nguo nyepesi zinazoonyesha uchi wake, kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amgeukie na kumwambia:

”Funika kila kitu isipokuwa uso na mikono.”

Maana yake ni kwamba aliingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa amefunua vitu vingine kama kichwa, kifua, mguu au mfano wa hayo.

Kwa hiyo sababu hii ya tano inaonekana kwa mwenye kutafakari matini. Kwa hivyo matini kwa maana hii inakuwa ni munkar na isiyofaa kutokea kwa Asmaa´ (Radhiya Allaahu ´anhaa), ambaye ni mwanamke mwema anayejulikana kwa kheri. Isitoshe ni mke wa az-Zubayr, ambaye ni katika watu wenye wivu mkubwa katika dini ya Allaah, baba yake as-Swiddiyq, ambaye ni mkamilifu zaidi wa waumini kwa imani na mbora wao baada ya Manabii (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

Kwa hiyo as-Swiddiyq ni mbora wa Maswahabah na ndiye kiongozi wao baada ya Manabii. Basi inawezekanaje kwa msichana huyu mtukufu mwema, msichana wa as-Swiddiyq na mke wa az-Zubayr kuingia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika nguo nyepesi zinazoonyesha uchi wake, kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amgeukie na kumwambia kadhaa na kadhaa?

Hili kwa tunavyoamini halikutokea. Bali ni tukio la uongo na batili.

[1] 33:53

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3484/اسباب-ضعف-حديث-كشف-الوجه-والكفين
  • Imechapishwa: 24/11/2026