Swali: Je, kuvaa pete ni Sunnah au ni jambo la kuruhusiwa tu pamoja na kututajia dalili?

Jibu: Hatufahamu dalili inayoonyesha kuwa kuvaa pete ni Sunnah. Lililo dhahiri zaidi ni kuwa ni jambo la kuruhusiwa. Maswahabah walivaa pete. Miongoni mwao wapo waliovaa na wapo walioacha. Hivyo kuvaa pete, khaswa pete ya fedha kwa mwanaume, kinachoonekana karibu zaidi na usahihi ni kuwa ni katika mambo yaliyoruhusiwa tu. Imekuja katika baadhi ya Hadiyth yanayojulisha kuwa pete ni kwa ajili ya mtawala, kama Hadiyth ya Abu Rayhaanah na cheni yake ya wapokezi iko karibu. Dhahiri yake inaonyesha kuwa huvaliwa na mtawala. Lakini Hadiyth Swahiyh pia zinafahamisha kuwa kuvaa pete kunajuzu kwa wanaume kwa ujumla, hata kama si mtawala. Hadiyth hizo ni Swahiyh zaidi kuliko Hadiyth ya Abu Rayhaanah. Hata kama Hadiyth ya Abu Rayhaanah itasihi, basi inakuwa ni yenye kupingana na zilizo Swahiyh inapokuja kwa upande wa matini, licha ya kwamba katika cheni yake kuna baadhi ya maneno. Kwa kifupi yaliyo sahihi ni kwamba inajuzu kwa wanaume kuvaa pete ya fedha. Lakini ni kwa njia ya kuruhusu, si kwa njia ya kwamba ni Sunnah.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1384/حكم-لبس-الرجل-للخاتم
  • Imechapishwa: 05/04/2026