Ni lazima kutekeleza adhabu ya kidini hadharani?

Swali: Je, inashurutishwa wakati wa kutekeleza adhabu iwe mbele ya watu au inawezekana kutekelezwa gerezani bila kutangazwa, kama kwa mfano kumpiga mnywaji wa pombe?

Jibu: Mtawala anapaswa kufanya lililo bora zaidi. Allaah amesema:

وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ

”Washuhudie adhabu yao kundi la waumini.”[1]

Ikiwa ataitekeleza gerezani, katika jumba, mahali pa wazi kwa watu au sehemu yoyote ikiwa itahudhuriwa na kundi la watu, basi lengo linakuwa limetimia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwahi kutekeleza adhabu ya pombe kwa mnywaji ndani ya nyumba yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati walipoletwa kwake akawaamuru wapigwe humohumo. Makusudio ni kwamba mtawala anafanya lililo bora zaidi. Ikiwa lililo bora ni kuonyesha kwa watu ili waogope na wajiepushe, basi afanye hivyo. Anachagua jambo lenye kuzuia maovu kwa watu katika sehemu inayofaa na ihudhuriwe na kundi la waislamu, hata kama si wengi. Kundi linatosha.

Swali: Vipi ikiwa kusudio ni kuzingatia hisia za huyu mhalifu anayetekelezewa adhabu?

Jibu: Hapana, kinachopaswa kuzingatiwa ni maslahi ya watu na maslahi ya ummah. Mtawala anapaswa kuzingatia maslahi ya ummah ambayo ndani yake kuna kuzuia batili na kusimamisha haki. Ikiwa kiongozi ataona kuwa kwa mujibu wa ijtihadi yake ya Kishari´ah ni bora mtu huyu apewe adhabu ya kuaziriwa mahali fulani au ahadhibiwe kwa adhabu mahali fulani, basi hakuna ubaya. Hili linarejea kwenye ijtihadi yake, ikiwa si kwa matamanio bali kwa jambo linalokusudiwa Kishari´ah.

[1] 24:02

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3336/حكم-اقامة-الحدود-امام-الناس
  • Imechapishwa: 30/09/2026