Ni ipi hukumu ikiwa mswaliji ataacha al-Faatihah kwa makusudi au kwa kusahau?

Swali: Ni ipi hukumu ikiwa mtu ataacha al-Faatihah kwa makusudi au kwa kusahau katika swalah ya kusoma kwa sauti ya juu au ya kusoma kimyakimya?

Jibu: Kama akiwa ni maamuma, hilo halimdhuru ikiwa ni mjinga au amesahau, kwa sababu ni wajibu kwake lakini hudondoka kwa ujinga na kusahau. Vilevile inadondoka ikiwa atakuja na imamu akiwa katika Rukuu´ na Rak´ah inamtosheleza. Lakini ikiwa ni imamu au mwenye kuswali peke yake, haidondoki. Kwa maana ya kwamba akisahau katika Rak´ah moja, Rak´ah nyingine inatakiwa kusimama nafasi yake na huongeza Rak´ah nyingine. Akitoa salamu na kukapita muda mrefu, basi atairudia swalah yake upya kwa sababu ni nguzo kwa upande wa imamu na mwenye kuswali peke yake. Ni lazima isomwe. Akiisahau katika Rak´ah moja, Rak´ah nyingine inatakiwa kuletwa mahali pake na aswali Rak´ah nyingine ili akamilishe. Lakini kwa maamuma ni wajibu kwake, lakini inadondoka kwa kusahau na kughafilika, na pia inadondoka kwa kuikosa ikiwa atakuja na kumkuta imamu amesharukuu, katika hali hiyo atarukuu pamoja naye na Rak´ah hiyo itamtosheleza, kama ilivyokuja katika Hadiyth ya Abu Bakrah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30931/ما-حكم-ترك-الفاتحة-في-الصلاة-عمدا-او-سهوا
  • Imechapishwa: 13/09/2025