Swali: Ni ipi hukumu ya kukaa na watu wasiokuwa wanaswali, ingawa ni jamaa zetu? Ni ipi hukumu ya kuzuru makaburi?

Jibu: Ama jamaa zako wasiokuwa wanaswali, hawa ni wajibu kuwakatia uhusiano, usiwatembelee, wasikutembelee, usiwaalike kwenye karamu ya ndoa na wala usikubali mwaliko wao. Bali unatakiwa kuwahama mpaka Allaah awaongoze na waanze kuswali, kwa sababu kuacha swalah ni kosa kubwa sana. Bali ni ukafiri na upotofu, kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ahadi iliyopo baina yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi yeyote atakayeiacha amekufuru.”

“Baina ya mtu na ukafiri na shirki ni kuacha swalah.”

Kwa hiyo ni wajibu wako kuwahama na kujitenga nao, isipokuwa wakikubali nasaha. Basi unatakiwa kuwapa nasaha na kuwabainishia kwamba wamefanya kosa kubwa, ukafiri wa wazi na shari kubwa. Uwanasihi na uwabainishie makosa yao, huenda Allaah akawaongoza kupitia wewe. Kadhalika uwahimize wale wenye kauli inayosikilizwa kwao wawanasihi na kuwaelekeza kwenye kheri. Wakikubali, ni vyema. Vinginevyo ni wajibu kuwahama mpaka watubie kutokana na tendo hili baya.

Ama kuzuru makaburi kwa ajili ya kuwaomba waliokufa au kuomba msaada kwao, huo ni ukafiri mkubwa na ni shirki kubwa. Wale wanaowatembelea wafu kama wanaomzuru al-Husayn huko Misri, ´Abdul-Qaadir huko ´Iraaq au wengineo ambapo wakawaomba wakidhi haja au msaada, huo ni ukafiri mkubwa. Vivyo hivyo katika nchi yoyote, anayezuru wafu kwa kuwaomba mahitaji, kuomba kuponywa maradhi au msaada, huo ni ukafiri mkubwa. Hii ndiyo dini ya washirikina wa mwanzo. Hii ndiyo dini ya makafiri wa Quraysh. Tunaomba Allaah atulinde.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3302/حكم-مجالسة-اقارب-لا-يصلون-ودعاء-الموتى
  • Imechapishwa: 05/10/2026