Swali: Hakika mazingira yetu ya leo yamejaa misukosuko, uharibifu, Bid´ah na maovu. Basi tunayasahihishaje mazingira haya? Hadi lini tutaendelea kuweka vichwa vyetu kwenye mchanga?

Jibu: Mazingira ndiyo uwanja wa matendo, uwanja wa ulinganizi na uwanja wa nasaha. Hivyo ni wajibu kwa mwenye kuwa na elimu kuitoa katika Khutbah, maandishi na mihadhara ili ajitahidi kueneza dini ya Allaah na atekeleze sehemu yake katika hilo. Asifiche kichwa chake kwenye mchanga wala asijifiche. Bali ni wajibu kwa kila mwenye elimu afanye kazi, ajitahidi, aseme haki na aisambaze haki.

Kwa hakika, kwa fadhilah za Allaah, wapo sasa wanaotekeleza jukumu hili na wanaojitahidi kulifanya katika nchi nyingi na sehemu nyingi. Wanajitahidi kueneza dini ya Allaah, wanajifunza na wanatafakari elimu katika vyuo ambavyo havifundishi dini, bali hufundisha uhandisi, tiba na fani nyinginezo. Hata hivyo miongoni mwa wanafunzi wake wamejitokeza wanafunzi wema wanaoitafuta dini ya Allaah, wanaisimamia haki na wanawalingania watu, mbali na wanafunzi walioko katika vyuo vingine vinavyohusiana na Shari´ah, misingi ya dini, na vyuo vya ulinganizi na mengineyo. Na wapo wengine ambao hawapo katika vyuo kabisa, bali wamejifunza katika misikiti, wamejifunza kutoka kwa wanazuoni, wamesoma Kitabu cha Allaah na wakasoma walichoweza katika Sunnah zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakahudhuria vikao vya elimu, wakafaidika na wakawa na juhudi kubwa katika kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kuwaelekeza watu katika kheri. Nao wanaongezeka na wanazidi kuenea.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1497/ضرورة-الدعوة-الى-الله
  • Imechapishwa: 03/04/2026