97. Ikiwa haki iko pamoja na wazushi, basi kuna makosa ndani ya Qur-aan na Sunnah

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Kwa hivyo ikiwa haki iko pamoja na hawa wanaopinga na kukanusha sifa zilizothibiti ndani ya Qur-aan Sunnah kwa matamshi haya na mfano wake kinyume na yale yanayopata kufahamika kutoka ndani ya Qur-aan na Sunnah, ima kwa andiko la wazi au udhahiri umefahamisha hivo, ni vipi basi itafaa kwa Allaah (Ta´ala), kisha Mtume Wake, kisha wabora wa ummah daima kuzungumza kwa mambo isiyokuwa dalili ya wazi au udhahiri umefahamisha hivo kinyume na ile haki ambayo ni wajibu kuiamini?

MAELEZO

Anachomaanisha ni kwamba ikiwa haki kuhusu majina na sifa za Allaah iko na wale watu waliokuja nyuma ya kwamba haijuzu kumnasibishia Allaah, kwamba haitakiwi kumsifu Allaah kwazo wala kuitwa kwa majina hayo, hiyo maana yake ni kuwa Qur-aan na Sunnah havikuja kuwaongoza watu, bali vimekuja kuwapotosha. Kwa sababu Qur-aan na Sunnah vinafahamisha kinyume na yale yanayosemwa na watu hawa. Kwa hivyo ikiwa haki iko pamoja nao, basi Qur-aan na Sunnah vimekuja kuwapotosha na kuwadanganya watu. Inatosha tuhuma hii kuwa ni upotofu na kufuru. Ima haki iwe ni yale yanayofahamishwa na Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya ummah, jambo ambalo ndio jambo la kukata kabisa na yakini, au haki iko pamoja na watu hawa, jambo ambalo linapelekea kuwa yaliyomo ndani ya Qur-aan na Sunnah ni batili. Hakuna uwezekano mwingine wa tatu. Kwa mujibu wa uwezekano wa pili ni kwamba Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waumini walisema yasiyokuwa haki na wakaficha haki ambayo baadaye imebainishwa na Jahmiyyah na Mu´tazilah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 140
  • Imechapishwa: 01/09/2024