89. Kursiy ya Allaah ni yenye kutoa sauti

85 – Abu Muusa (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Kursiy ni mahali pa kuwekea Miguu miwili. Inatoa sauti kama sogi.”[1]

Ameipokea al-Bayhaqiy katika ”al-Asmaa´ was-Swifaat”. Kutoa sauti hakuna mahusiano yoyote na Sifa. Ni kama kutikisika kwa ´Arshi kwa kufariki kwa Sa´d, kupasuka kwa mbingu siku ya Qiyaamah na mfano wa hayo. Tunaomba kinga kwa Allaah kutokana na kuyazingatia hayo kuwa ni katika sifa za Allaah (´Azza wa Jall). Zingatia pia kwamba hakuna dalili iliyothibiti iliyotaja kuhusu kutoa sauti.

[1] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Ameipokea pia ´Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal katika “as-Sunnah”, uk. 71, Abuush-Shaykh katika “al-´Adhwamah” (2/42) na Abu Ja´far bin Abiy Shaybah katika “al-´Arsh”, uk. 436-437. Wasimulizi wake wote ni wenye kuaminika na wanaotambulika.

al-Kawthawriy, ambaye anajulikana kupinda kwake kutokana na Ahl-us-Sunnah  wal-Jamaa´ah, amekosea katika maelezo yake ya chini ya ”al-Asmaa´ was-Swifaat”, uk. 404 kwa sababu ya kuwepo kwa ´Umaarah bin ´Umayr katika cheni yake ya wapokezi na akasema kuwa ”al-Bukhaariy amemtaja katika ”adh-Dhwu´afaa´”. Hili ni kosa la wazi. Kwa kweli sijui kama amefanya hivo kwa kuteleza au amekusudia. Tumeona kuwa bwana huyu anafanya makosa ya mabishano ambayo yanafanana na uwongo bali uwongo kabisa, kama alivyobainisha hilo ´Allaamah al-Yamaaniy katika Radd yake kubwa dhidi yake kwa jina at-Tankiyl bi maa fiy Ta’niyb al-Kawthariy min al-Abaatwiyl”. Haya nayasema kwa sababu kuna maafikiano kwamba ´Umaarah bin ´Umayr ni mwanafunzi wa Maswahabah ambaye ni mwenye kuaminika. al-Bukhaariy na Muslim wamemnukuu katika ”as-Swahiyh” zao. Haafidhw Ibn Hajar amesema kwamba alikuwa ”madhubuti na imara”. Sidhani kama mtu kama al-Kawthariy anaweza kutojua jambo hilo. Isitoshe hayuko kabisa katika ”ad-Dhwu´afaa” ya al-Bukhaariy, tofauti na alivyodai. Lakini aliyetajwa humo ni ´Umaarah bin Juwayn – ambaye ni mwenye kuachwa. Tunakuomba msamaha, ee Allaah!

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Uluww lil-´Aliy al-Ghaffaar, uk. 107
  • Imechapishwa: 03/07/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy