Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَحَلَّ اللَّـهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا

”Allaah amehalalisha biashara na ameharamisha ribaa.”[1]

Biashara ni kubadilishana mali kwa mali. Inajuzu kuuza kila kitu kinachomilikiwa ambacho ndani yake kuna manufaa yaliyoruhusiwa, isipokuwa tu mbwa, kwani haijuzu kumuuza na wala hakuna fidia juu ya yule anayemuangamiza. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza thamani ya mbwa na akasema:

“Yule mwenye kufuga mbwa, isipokuwa mbwa wa mifugo au wa kuwinda, hupunguziwa katika matendo yake kila siku sawa na milima miwili.”[2]

Haijuzu pia kuuza kitu ambacho si mali ya muuzaji, isipokuwa kwa idhini ya mwenye mali hiyo au ikiwa ana mamlaka juu yake.

Haijuzu pia kuuza kitu ambacho hakina manufaa, kama wadudu, wala kitu ambacho manufaa yake ni haramu, kama pombe na mnyama aliyekufa.

Haijuzu pia kuuza kitu kisichojulikana, kama kile kitakachobebwa na mjakazi wake au kitakachozalishwa na mti wake, wala kitu kisichojulikana kama mimba iliyo tumboni, na kitu kilichopo mbali ambacho hakijaelezwa wala hakijaonekana hapo kabla. Wala haijuzu kuuza kitu ambacho hawezi kukikabidhi, kama mtumwa aliyekimbia, mnyama aliyepotea, ndege aliye angani na samaki aliye majini.

Wala haijuzu kuuza mali iliyonyakuliwa isipokuwa kwa yule aliyeinyakua au kwa mwenye uwezo wa kuichukua kutoka kwake.

Wala haijuzu kuuza kitu kisichoainishwa, kama kusema nimemuuza mtumwa mmoja miongoni mwa watumwa wangu au kondoo mmoja miongoni mwa kundi langu, isipokuwa katika kitu ambacho sehemu zake zinafanana, kama kipimo kutoka kwenye rundo la nafaka.

[1] 2:275

[2] al-Bukhaariy (5480) na Muslim (1574).

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 52
  • Imechapishwa: 16/11/2026