Maswahabah wamegawanyika katika mafungu mawili:

1 – Muhaajiruun. Hao ni wale walioziacha nchi na miji yao na wakakimbia kwa dini yao. Walihajiri kwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakaishi naye Madiynah na wakapambana jihaad bega kwa bega pamoja naye.

2 – Answaar. Hao ni wakazi wa Madiynah na walikuwa wanatokana na kabila la al-Aws na al-Khazraj. Walifungua mji wao, majumba yao na mali zao kwa ajili ya ndugu zao Muhaajiruun. Waliwapokea kidugu na kwa mapenzi:

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

“Wapatiwe pia mafuqara Muhaajiruun ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na mali zao wanatafuta fadhilah na radhi kutoka kwa Allaah na wanamnusuru Allaah na Mtume Wake – hao ndio wakweli.”[1]

Kisha Akawataja Answaar na kusema:

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ٌ

”Na wale waliokuwa na makazi [Madiynah] na wakawa na imani kabla yao wanawapenda wale waliohajiri kwao na wala hawahisi choyo yoyote vifuani mwao kwa yale waliyopewa [Muhaajiruun] na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe ni wahitaji. Na yeyote anayeepushwa na uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.”[2]

Halafu Akawasifu wale waliowafuata na akasema:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

”Na wale waliokuja baada yao wanasema: ”Ee Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[3]

Ama wale ambao wanawatukana Muhaajiruun na Answaar na wanawatuhumu kuwa hawana utambuzi juu ya majina na sifa za Allaah na kwamba wale waliokuja nyuma ndio wana utambuzi huo, hawakuwafuata kwa wema. Hawawatakii radhi wala kuwaombea msamaha.

[1] 59:8

[2] 59:9

[3] 59:10

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 95-96