58. Inajuzu kusoma Qur-aan kwa usiyo mpangilio wake

Ikiwa mtu atakwenda kinyume na mpangilio ambapo akachagua kusoma Suurah isiyofuata ile ya kwanza au akaenda kinyume na mpangilio ambapo akasoma Suurah kisha akasoma iliyo kabla yake, inajuzu. Kwa sababu kumepokelewa masimulizi mengi juu ya hilo. Imepokelewa kuwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alisoma katika Rak´ah ya kwanza ya swalah ya Fajr Suurah ”al-Kahf” na katika ya pili Suurah ”Yuusuf”.

Hata hivyo kundi la Salaf wamechukia kwenda kinyume na mpangilio wa msahafu. Ibn Abiy Daawuud amepokea kutoka kwa al-Hasan kwamba alikuwa akichukia kusoma Qur-aan isipokuwa kwa mpangilio wa msahafu. Amepokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh ya kwamba ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) aliambiwa:

”Fulani anasoma Qur-aan kwa kuipindua.” Akasema: ”Huyo ana moyo uliopinduka.”

Hata hivyo kusoma Suurah kuanzia mwisho wake kwenda mwanzo wake, hilo limekatazwa kwa msisitizo mkubwa, kwa sababu linaondoa baadhi ya aina za muujiza wa Qur-aan na kuharibu hekima ya mpangilio wa Aayah. Ibn Abiy Daawuud amepokea kutoka kwa Ibraahiym an-Nakha´iy, imamu mkubwa wa mwanafunzi wa Maswahabah na Imaam Maalik bin Anas kwamba walichukia hilo. Imaam Maalik alikuwa akiliona kuwa ni jambo kubwa na akisema ”hilo ni jambo kubwa”.

Ama kuwafundisha watoto kwa kuanza kutoka mwisho wa msahafu kwenda mwanzo wake, hilo ni jambo jema. Hili halipo katika mlango huu, kwa sababu ni usomaji uliogawanyika katika siku tofauti, na pia hurahisisha kuhifadhi kwao – Allaah ndiye Mjuzi zaidi.

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 23/11/2026