43. Zakaah ya vitu vitokavyo ardhini

Kuna sampuli mbili:

Sampuli ya kwanza ni mazao. Zakaah inawajibika katika kila punje na tunda linalotoka ardhini kwake, ambalo hupimwa kwa kipimo na kuhifadhiwa, ikiwa litafikia takriban kilogramu 653. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna zakaah katika punje wala tunda mpaka lifikie takriban kilogramu 653.”[1]

Zakaah ya sehemu ya kumi inawajibika katika yale yanayomwagiliwa na mvua, mito na maji yanayotiririka. Hata hivyo ikiwa mazao yanamwagiliwa maji kwa juhudi ya mwanadamu, basi inawajibika kutoa nusu ya sehemu ya kumi.

Dalili za kuiva zinapoonekana katika matunda na punje zinapokuwa ngumu, basi zakaah huwa imewajibika. Punje haitolewi zakaah isipokuwa ikiwa imetenganishwa na makapi, na tunda halitolewi zakaah isipokuwa likiwa limekauka.

Hakuna zakaah katika yale anayoyapata kutokana na punje na matunda yanayoruhusiwa kuchumwa, wala katika yale anayoyakusanya kutoka ardhini bila kulima, wala katika yale anayoyapata kama malipo wa kuvuna.

Aina moja haiunganishwi na aina nyingine ili kukamilisha kile kiwango kinachowajibisha zakaah. Ikiwa ni aina moja lakini punje au matunda yake ni za aina mbalimbali, kama tende, basi zakaah inawajibika ndani yake. Hutolewa zakaah ya kila aina kutoka katika aina hiyo. Hata hivyo ikiwa atatoa bora badala ya iliyo duni, inajuzu na atakuwa amefanya kwa khiyari yake.

Aina ya pili ni madini. Mwenye kutoa madini kutoka katika mgodi au kitu chenye thamani inayofikia kile kiwango kinachowajibisha zakaah, basi anapaswa kutoa zakaah. Kitu hicho kinaweza kuwa dhahabu, fedha au kile kinachochimbwa kwa thamani yake, kama vile vito,  kope, shaba, chuma au  madini mengineyo. Haitolewi zakaah isipokuwa baada ya kuyeyushwa na kusafishwa.

Hakuna zakaah katika lulu, marijani, ambergis na miski. Hakuna zakaah pia katika uwindaji wa nchi kavu na baharini.

Katika mali iliyopatikana kutoka katika hazina iliyozikwa tangu zama za kale, kunatolewa sehemu ya tano, pasi na kujali mali hiyo ni ya aina au kiwango gani. Sehemu hiyo ya tano hutumika kwa wale wenye kuiistahiki. Sehemu iliyobaki ni ya yule aliyeipata.

[1] Muslim (979).

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 36-37
  • Imechapishwa: 26/10/2026