41. Hali, jinsia na umri wa mnyama anayetolewa zakaah

Katika zakaah hachukuliwi mbuzi dume, mnyama mwenye kasoro ya jicho, mnyama mzee sana, mnyama mchanga ambaye bado hajafikia umri wa kuchukuliwa katika zakaah, mnyama mwenye mimba na wala mnyama aliyenenepa. Wala haichukuliwi mali iliyo mbaya zaidi, mali iliyo bora zaidi na yenye thamani zaidi, isipokuwa ikiwa wenye mali watajitolea kuitoa.

Kinachotolewa si chochote isipokuwa mnyama wa kike aliye mzima, isipokuwa katika ng´ombe thelathini, ambapo ng´ombe dume mwenye mwaka mmoja anatosheleza. Ngamia dume mwenye miaka miwili anatosheleza badala ya ngamia jike mwenye mwaka mmoja ikiwa huyo hakupatikana. Isipokuwa ikiwa mifugo yote ni madume au ni wagonjwa – katika hali hiyo mmoja katika mifugo hiyo anatosheleza kumtoa.

Katika kondoo hatolewi isipokuwa kondoo aliyefikisha umri wa miaka miwili au mbuzi aliyefikisha umri wa mwaka mmoja. Umri uliotajwa ndio unaotakiwa kutolewa, isipokuwa ikiwa mwenye mali atachagua kutoa mnyama mwenye umri mkubwa zaidi kuliko ule unaowajibika au ikiwa mifugo yote ni midogo, basi atatoa mnyama mdogo.

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 36
  • Imechapishwa: 26/10/2026