´Aqiydah inatakiwa kutendewa kazi. Wengi hii leo wanaijahili na wanaidharau. Wanasema kuwa waislamu ni waislamu na inatosha na kwamba mtu hatakiwi kuzihoji ´Aqiydah zao. Aidha wanasema kuwa tunafarikisha kati ya watu. Tunawajulisha kuwa sio sisi tunaofarikisha kati ya watu. Sisi tunalingania katika umoja na kuirekebisha ´Aqiydah. Hatulinganii katika mfarakano, lakini tunalingania katika kukusanyika juu ya haki. Wingi pasi na ´Aqiydah hauna faida yoyote. Ni lazima kuwa na umoja, lakini sisi tunapenda umoja wa wengi juu ya ´Aqiydah. Kuna faida gani ikiwa wingi ni pasi na ´Aqiydah? Hakuna faida yoyote. Sisi tunawatakia watu kheri na wakusanyike. Hatutakiwi wafarikiana ambapo kila mmoja anafanya na kuamini kile akitakacho na kusema kuwa watu wako huru katika ´Aqiydah zao. Ni nani mwenye kusema kuwa watu wako huru katika ´Aqiydah zao? Mambo yangelikuwa hivo basi Allaah asingewatumiliza Mitume na akateremsha Vitabu. Ingelikuwa kila mmoja anachukua uhuru wake na hivyo kuingia kwenye upotofu. Lakini watu wameamrishwa kumwabudu Allaah pekee. Huu ndio uhuru. Uhuru ni katika kumwabudu Allaah pekee, utumwa ndio unapatikana katika kumwabudu mwengine asiyekuwa Allaah. Ibn-ul-Qayyim amesema:

Wamekimbia mbali na utumwa ambao wameumbiwa

na wakajaribiwa kwa utumwa wa nafsi na wa shaytwaan[1]

Utumwa ambao wameumbiwa ni kumwabudu Allaah pekee. Utumwa huo ndio una kuwatengeneza watu, uokozi na kheri yao. Wakati walipoukimbia ndio wakaingia katika utumwa wa shaytwaan na nafsi, jambo ambalo ndio utwevu na udhalilifu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na wanadamu isipokuwa waniabudu.”[2]

نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ

“Wajulishe waja Wangu kwamba: Hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu na kwamba adhabu Yangu ndiyo adhabu iumizayo.”[3]

[1] an-Nuuniyyah (2/466).

[2] 51:56

[3] 15:49-50

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 57-58
  • Imechapishwa: 31/07/2024