Miongoni mwa fadhilah zake pia ni athari njema anazoziacha swawm ambazo zinapendwa na Allaah, nazo ni kubadilika kwa harufu ya mdomo wa mwenye kufunga kutokana na swawm. Hizi ni athari zilizotokana na utiifu na hivyo ikawa inapendwa mbele ya Allaah (Ta´ala):

”Harufu ya mdomo wa mwenye kufunga mbele ya Allaah ni bora zaidi kuliko harufu ya miski.”

Miongoni mwa fadhilah za swawm ni kwamba Allaah Amewatenga wenye kufunga kwa mlango maalum miongoni mwa milango ya Pepo ambao hawaingii isipokuwa wao tu hali ya kuwa ni heshima na utukufu kwao. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Sahl bin Sa´d (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika Peponi kuna mlango unaoitwa ´Rayyaan`. Wataingia kupitia humo wenye kufunga siku ya Qiyaamah; hawaingii kupitia huo mtu mwingine yeyote. Itasemwa: ”Wako wapi wenye kufunga?” Watasimama na kuingia. Watakapoingia utafungwa na wala hatakuingia tena mtu mwingine.”[1]

Miongoni mwa fadhilah za swawm ni kwamba humkinga mwenye kufunga dhidi ya madhambi yanayomdhuru, humlinda dhidi ya matamanio yenye madhara na humkinga dhidi ya adhabu ya Moto. Kama ilivyokuja katika Hadiyth kwamba funga ni kinga madhubuti, kwa maana nyingine ni sitara imara dhidi ya khatari hizo.

Miongoni mwa fadhilah za swawm ni kwamba du´aa ya mfungaji hukubaliwa. Ibn Maajah na al-Haakimwamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar ambaye amesimulia ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika mwenye kufunga anayo du´aa wakati wa kufungua ambayo hairudishwi nyuma.”[2]

Allaah (Ta´ala) amesema katikati ya Aayah zinazozungumzia swawm:

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ

“Watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi niko karibu Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba.”[3]

Aayah hii inawahimiza wafungaji kuomba du´aa kwa wingi.

[1] al-Bukhaariy (1896) na Muslim (1152).

[2] Ibn Maajah (1753) na al-Haakim (01/422).

[3]2:186

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 29
  • Imechapishwa: 21/02/2026