Mushabbihah ni wale ambao wamezifananisha sifa za Allaah na sifa za viumbe.

Mu´tazilah ni wale ambao wamezikanusha sifa Allaah. Hoja yao eti wanamtakasa Allaah kutokana na mapungufu. Matokeo yake wakapetuka katika jambo hilo. Ni wafuasi wa Waaswil bin ´Atwaa´ na ´Amr bin ´Ubayd, wawili hao walikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa al-Hasan al-Baswriy na walikuwa wakihudhuria katika duara zake za kielimu. Wakati al-Hasan al-Baswriy alipoulizwa kuhusu mtenda dhambi kubwa na akajibu kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah, kwamba Allaah ndiye atakayeamua cha kumfanya na hakufuru kwa dhambi hiyo kubwa ijapo imani yake ni dhaifu, hapo ndipo Waaswil alipomkemea na kumwambia kuwa yuko katika ngazi kati ya ngazi mbili – sio kafiri wala muislamu. Akazua ´Aqiydah hii batili. Matokeo yake akajitenga (اعتزل) na masomo ya al-Hasan. Wakakusanyika kwake watu ambao wana fikira moja kama yake, na wakaunda kikundi ambacho kikaitwa Mu´tazilah (المعتزلة).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 264-265
  • Imechapishwa: 27/05/2025