24. Kuamini adhabu ndani ya kaburi

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini adhabu ya kaburi.”

MAELEZO

Adhabu au neema za ndani ya kaburi ni kitu kisichojua yeyote isipokuwa Allaah. Ndani ya kaburi ima yule maiti atahisi maumivu au atastareheka. Adhabu na neema za ndani ya kaburi ni jambo limethibiti kwa mapokezi mengi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau msingelikufa basi ningemuomba Allaah akusikilizisheni adhabu ya ndani ya kaburi.”[1]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipita karibu na makaburi mawili akasema:

“Hakika wawili hawa wanaadhibiwa, hawaadhibiwi kwa jambo kubwa. Bali ni jambo kubwa. Ama kuhusu mmoja wao alikuwa akieneza uvumi na mwengine alikuwa hajikingi na cheche za mkojo.” Kisha baada ya hapo akachukua kuti na mtende na akalipasua mara mbili na akayasimika kwenye makaburi yale. Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Kwa nini umefanya hivo?” Akajibu: “Huenda wakakhafifishiwa adhabu midhali bado ni hayajakauka.”[2]

Katika Hadiyth ya al-Baraa´ bin ´Aazib (Radhiya Allaahu ´anh) kuna yenye kufahamisha hivo. Kadhalika miongoni mwa neema za kaburi ni ile Hadiyth isemayo:

“Roho zao ziko ndani ya matumbo ya kijani ya ndege. Ziko na mataa yaliyotundikwa kwenye ´Arshi. Zinaruka huku na kule Peponi zinapotaka. Halafu zinarudi kwenye kwenye lile taa.”[3]

Kama tulivosema kuna dalili nyingi zinazothibitisha neema na adhabu ndani ya kaburi.

Kuna ambao wamedai kwamba adhabu ya ndani ya kaburi haingii akilini kwa vile akili yao haiwezi kulifikiria hilo. Wanasema kwamba iwapo tutafukua lile kaburi basi tutakuta kuna mifupa mikavu na kwamba hatutoona alama wala athari yoyote ya neema wala adhabu. Hivo ndivo wanavosema Mu´tazilah na vifaranga vyao wa leo kama Hizb-ut-Tahriyr.

Wanachuoni wametofautiana kama adhabu ya kaburi inakuwa kwenye roho peke yake, kiwiliwili peke yake au vyote viwili. Maoni yaliyo karibu zaidi na usawa ni kwamba adhabu na neema inakuwa katika roho na kiwiliwili na kwamba kiwiliwili kinapata adhabu na neema kama jinsi roho inavyopata.

[1] Muslim (2867).

[2] al-Bukhaariy (218) na Muslim (292).

[3] Muslim (1887).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 119-120
  • Imechapishwa: 23/04/2019