170 – Dini ya Allaah ardhini na mbingu ni moja tu, nayo ni Uislamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

”Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.”[1]

وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”… na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.”[2]

MAELEZO

Uislamu ni kumwabudu Allaah pekee, asiyekuwa na mshirika. Hili ndilo ambalo Malaika mbinguni, watu na majini ardhini wanamwabudu Allaah kwalo. Huo ndio Uislamu. Katika kitabu “al-Usuwl ath-Thalaathah” Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amethibitisha utambulisho wa kuenea kwamba ni kujisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujiepusha na shirki. Uislamu ndio dini ya Mitume wote na wafuasi wao. Kila Mtume aliwalingania watu wake katika jambo hilo. Kila ambaye aliwafuata katika jambo hilo anazingatiwa kuwa muislamu, pasi na kujali wakati gani, kwa sababu wamejisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha na kunyenyekea Kwake kwa kumtii. Dini ya Mitume ni moja, lakini Shari´ah zao zinatofautiana kutokana na mahitaji ya watu katika kila zama na maeneo. Imekuja katika Hadiyth:

“Mitume ni ndugu kutoka kwa mama tofauti. Mama zao wanatofautiana lakini dini yao ni moja.”[3]

Allaah (Ta´ala) amesema:

لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا

“Kwa kila Ummah katika nyinyi Tumeujaalia Shari’ah na mfumo wake.”[4]

Allaah anamuwekea Shari´ah kila Mtume yale yanayonasibiana na watu wake na kunasibiana na manufaa yao. Baada ya hapo anayafuta kutegemea na manufaa ya watu hao waliokuja. Ambaye alikuwa anafuata dini ya Mtume fulani kabla ya kufutwa, basi huyo ndiye muislamu. Kipindi hicho Allaah anaabudiwa kwa yale aliyomuwekea Shari´ah Mtume huyo, lakini baada ya kutumilizwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) dini ikabaki ni moja na Shari´ah nyenginezo zote zilizotangulia zikafutwa. Dini yenye kuzingatiwa ikabakia dini yake Muahammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo haijuzu kwa yeyote kubakia juu ya dini yoyote miongoni mwa zile dini zilizotangulia. Kwa sababu ujumbe na dini yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni yenye kuenea kwa viumbe wote na ni yenye kufanya kazi katika kila kipindi na kila maeneo. Uislamu ndio dini ambayo Allaah amewaridhia waja Wake, kuanzia wakati alipotumilizwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka siku ya Qiyaamah.

[1] 3:19

[2] 5:3

[3] al-Bukhaariy (3443) na Muslim (1837).

[4] 5:48

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 257-258
  • Imechapishwa: 07/05/2025