13. Du´aa ya kujilinda kwa Allaah na kushindwa, uvivu, woga, ubakhili, hamu n.k.

52 – Zayd bin Arqam (Radhiya Allaahu ´anh) amesema: “Sikwambieni isipokuwa vile ambavo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema: “Alikuwa akisema:

اللهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ العَجْزِ وَالكَسَلِ، والبُخْلِ وَالهَرم، وعَذَاب الْقَبْر، اللَّهُمَّ آتِ نَفْسِي تَقْوَاهَا، وَزَكِّهَا أَنْتَ خَيرُ مَنْ زَكَّاهَا، أَنْتَ ولِيُّهَا وَموْلاَهَا، اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عِلمٍ لا يَنْفَعُ، ومِنْ قَلْبٍ لاَ يخْشَعُ، وَمِنْ نَفْسٍ لاَ تَشبَعُ، ومِنْ دَعْوةٍ لا يُسْتجابُ لهَا

 “Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kutokana na kushindwa, uvivu, woga, ubakhili, hamu na adhabu ya kaburi. Ee Allaah! Ipe nafsi yangu uchaji wake, itakase, kwani hakika Wewe ndiye mbora wa kuitakasa, Wewe ndiye Bwana na Mlinzi Wake. Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kutokana na elimu isiyonufaisha, moyo usionyenyekea, nafsi isiyoshiba na kutokana na du´aa isiyoitikiwa.”[1]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ipe nafsi yangu uchaji wake… “

Ipe nafsi yangu matendo mema ambayo yataifanya kumcha Allaah. Itakase maana yake ni kwamba aitwahirishe kutokana na uchafu wa maasi na iwafikishe katika tawbah ya kweli ambayo inamsafisha mtu kutokana na madhambi. Wewe ndiye Bwana na Mlinzi Wake ni kufanya Tawassul kwa Allaah. Allaah (Ta´ala) ndiye Mlinzi wa waumini.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kutokana na elimu isiyonufaisha… “

Hiyo ni ile elimu ambayo mwenye nayo haitendei kazi au elimu yenye kumdhuru, kama vile elimu ya uchawi na mfano wa elimu kama hizo.

Kinga dhidi ya moyo usionyenyekea bi maana moyo usiomnyenyekea Allaah na usiokuwa na utulivu.

Kinga dhidi ya nafsi isiyotosheka kunakusudiwa kuomba ulinzi kutokana na ubakhili, tamaa, ulafi na nafsi kufungamana na matumaini yaliyo mbali.

Kinga dhidi ya du´aa isiyoitikiwa udhahiri wa kuenea kwa du´aa ni kwamba anamuomba Allaah amuitikie du´aa yake hii na nyenginezo.

[1] Muslim (2722).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 15/10/2025