Swali: Nilivaa soksi baada ya kuosha mguu wa kushoto, kisha nikavaa, kisha nikaosha wa kulia na nikavaa soksi?

Jibu: Huenda ni kinyume chake: ameosha mguu wa kulia, kisha akavaa soksi, kisha akaosha wa kushoto na akavaa soksi. Hivi ndivyo watu wengi wanavyofanya.

Mwanafunzi: Je, jambo hili haliharibu ukamilifu wa twahara yangu?

Ibn Baaz: Baadhi ya wanazuoni wametaja kwamba ikiwa mtu ameosha mguu wa kulia, kisha akavaa soksi za ngozi au soksi za kawaida, kisha akaosha mguu wa kushoto, kisha akavaa pia, basi amevaa mguu wa kulia kabla twahara haijakamilika. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika mimi nimeziingiza nikiwa na twahara.”

Kwa hiyo wanazuoni wamesema kwamba sharti la kusahihika kupangusa juu ya soksi za ngozi ni miguu kuingizwa katika twahara kamili. Kwa msingi huo baadhi yao wamesema kwamba haifai kupangusa juu ya twahara hiyo mpaka avue mguu wa kulia kisha avae tena. Akivua mguu wa kulia baada ya kuosha wa kushoto kisha akavaa tena, basi kuvaa kwake kutakuwa juu ya twahara kamili. Hii ni tahadhari nzuri. Ikiwa mtu amevaa soksi ya kulia au soksi za ngozi, kisha akaosha wa kushoto na akavaa, basi ilivyo na tahadhari ni avue ya kulia kisha avae tena ili kuvaa kwake kuwe juu ya twahara kamili. Lakini asipofanya hivyo basi maoni sahihi ni kwamba twahara yake inatosha. Haya ndio maoni ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) na kundi la wanazuoni amnbao wamesema kwamba twahara wakati wa kuvaa ya kulia tayari ilikuwa karibu kukamilika na mtu alikuwa kwenye hukumu ya watwaharifu kwa sababu twahara ilikuwa ikiendelea na ilikamilishwa papohapo kwa njia ya Kishari´ah. Hivyo inasihi na hakuna ulazima wa kuvua tena mguu wa kulia na kuvaa upya. Hata hivyo akivua kisha akavaa upya ili kutoka kwenye makinzano ya wanazuoni na ili kuvaa kuwa juu ya twahara kamili, basi hilo ni jambo jema na linamuepusha na subuha, shaka na makinzano.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1113/لبس-الجورب-للرجل-اليمني-قبل-غسل-الرجل-اليسرى
  • Imechapishwa: 08/06/2026