Kuhifadhi maeneo katika safu msikitini II

Swali: Baada ya swalah ya ´Aswr huja watu na wanahifadhi nafasi katika msikiti mkuu kwa ajili ya muhadhara, kisha wanaenda sokoni na nje ya msikiti. Kabla ya adhaana ya Maghrib wanarudi katika nafasi zao walizozihifadhi. Je, kitendo hiki ni sahihi?

Jibu: Haijuzu kazi hii. Kuhifadhi nafasi katika safu ya kwanza kisha anaondoka, hapana. Hili halijuzu. Safu ya kwanza ni kwa yule aliyesonga mbele kwa nafsi yake, si kwa yule aliyesongesha viatu vyake, fimbo yake, chombo au kitu fulani. Hapana. Ni wajibu asonge mbele kwa nafsi yake na akae yeye. Akitanguliza fimbo yake, anayekuja anaiondoa na anakaa mahali pake. Hana haki ya kutanguliza kitu bila mwili wake. Kushindana ni kwa mwili; anasonga mbele na anakaa katika safu, anamtukuza Allaah, anamtaja, anasoma Qur-aan na anangojea swalah. Ama kuweka kitu na kwenda sokoni, kisha akija wakati wa adhaana anarudi, hili ni maovu na haijuzu. Ni wajibu kwa muislamu kuacha hilo. Aache safu ya kwanza kwa yule anayesonga mbele kwa nafsi yake ili akae katika safu na angojee swalah na asitangulie kwa fimbo tu au vitu vingine anavyoviweka katika nafasi yake. Tunamuomba Allaah awaongoze wote.

Swali: Vipi ikiwa ameenda kuchukua wudhuu´?

Jibu: Hili linafungua mlango. Aende akatawadha, akirudi, basi anakaa sehemu nyingine. Kwa sababu hili linafungua mlango, kila mmoja atajitetea kwa hili kwamba nilikwenda alienda kutawadha na nyudhuru nyinginezo. Yeye yuko juu ya nia yake njema. Kama si hivyo, basi yeye ndiye mwenye haki zaidi ikiwa alisimama kutawadha na hakukaa, lakini limempata jambo la dharurah. Ama aje akiwa hajatwaharika na aweke kitu, kisha aende kutawadha, hapana. Atawadhe kabla hajaja. Ama ikiwa alikuwa amekaa, lakini likampata jambo ambapo akaenda kutawadha, basi yeye ndiye mwenye haki zaidi kwa nafasi yake. Mwenye kuondoka katika sehemu yake kisha akarudi kwake, basi yeye ndiye mwenye haki nayo. Lakini baadhi ya watu hufanya hili hali ya kuwa hakwenda akiwa ametwaharika, bali alikuja akiwa na nia ya kuweka fimbo hii na kuondoka, jambo ambalo halifai.

Muulizaji: Vipi ikiwa alikuwa amekaa msikitini, kisha anasonga mbele au nyuma huku amehifadhi nafasi?

Ibn Baaz: Kwa nini anaondoka katika nafasi yake?

Mwanafunzi: Anataka kumtaja Allaah au kadhaa.

Ibn Baaz: Yote haya kuyaacha ni bora zaidi, kwa sababu yanafungua mlango kwa wengine. Akiyaacha, basi ni vyema. Hata kama atakuwa pembezoni mwa safu akija ni bora kuliko kuweka kitu. Si kwamba anakuwa anamiliki nafasi hiyo kwa sababu amesonga mbele, lakini kuondoka kwake kutoka safuni kunaweza kufungua mlango kwa wengine; kila mmoja atadai madai haya na yale. Mambo yatachanganyika na kutokea tatizo. Matokeo yake Bid´ah hii itaendelea kubaki.

Mwanafunzi: Ikiwa Allaah amekadiria amepatwa na upepo au haja ambapo akaenda na akarudi mahali pake hapana vibaya?

Ibn Baaz: Hakuna vibaya, ndiyo. Ikiwa alikaa mwanzo, alikuja akiwa ametwaharika ana nia ya kukaa, lakini likampata jambo hili. Ama mtu anayekuja kutoka nyumbani hana nia isipokuwa kuweka kitu na kuondoka, kwa maana hajatawadha kisha anaweka na kusema kuwa anaenda kutawadha, hili halifai.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3483/حكم-حجز-مكان-في-الصف-الاول
  • Imechapishwa: 23/11/2026