Wakati uko na dhiki, huzuni na msongo wa mawazo

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza ya kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema anapopatwa na dhiki:

لا إِله إِلاَّ اللهُ الْعَظِيمُ الْحَلِيمُ لاَ إِله إِلاَّ الله رَبُّ الْعَرْشِ العظيم لاَ إِلهَ إِلاَّ الله ربُّ السَّمواتِ وَرَبُّ الأَرض وَرَبُّ العرش الْكَرِيم

“Hakuna mungu anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, aliye Mtukufu Mpole. Hakuna mungu anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, Mola wa ´Arshi tukufu. Hakuna mungu anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, Mola wa mbingu, Mola wa ardhi na Mola wa ´Arshi tukufu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapohuzunishwa na jambo basi husema:

يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ برَحْمَتِكَ أَسْتَغِيثُ

“Ee Uliye hai! Ee Msimamizi wa kila kitu! Ninaomba msaada kwa rehema Zako.”[1]

Ameipoke at-Tirmidhiy.

Huyohuyo amepokea tena ya kwamba Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Ilikuwa wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapokuwa na wasiwasi juu ya jambo fulani, basi huinua kichwa chake mbinguni akisema:

سبحان الله العظيم

”Allaah ametakasika na mapungufu, Mtukufu!”

Anapojipinda katika kuomba du´aa husema:

يَا حَيُّ يَا قَيُّومُ

“Ee Uliye hai! Ee Msimamizi wa kila kitu!”[2]

Abu Bakrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Du´aa ya mwenye dhiki ni:

اللَّهُمَّ رَحْمَتَكَ أَرْجُو فَلاَ تَكِلْني إِلى نفسي طَرْفَةَ عَيْن وَأَصْلِح لِي شَأْنِي كُلَّهُ لا إِلهَ إِلاَّ أَنْتَ

“Ee Allaah! Nataraji rehema Zako. Usinitegemeze kwenye nafsi yangu japo kwa muda wa kukapua kwa jicho. Nitengenezee mambo yangu yote. Hapana mungu anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe.”[3]

Ameipokea Abu Daawuud.

Asmaa´ bint ´Umays (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia ya kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, nisikufundishe baadhi ya maneno ya kuyasema wakati wa janga?

الله الله رَبي لاَ أُشْرِكْ بِهِ شَيئاً

”Ee Allaah! Ee Allaah! Mola Wangu! Sikushirikishi na chochote.”[4]

Imekuja katika baadhi ya mapokezi mengine kwamba yanatakiwa kusemwa mara saba[5].

Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Dhuun-Nuun aliomba pindi alipokuwa tumboni mwa nyangumi:

لَّا إِلَهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ

“Hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe! Umetakasika! Hakika nilikuwa katika madhalimu.”

Hakuna muislamu anayeomba hivyo juu ya kitu isipokuwa Allaah humuitikia.”[6]

Ameipokea at-Tirmidhiy.

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Hakika najua neno ambalo hatolitamka aliyepatwa na dhiki isipokuwa Allaah atamfungulia; ni neno la ndugu yangu Yuunus (‘alayhis-Salaam).”

´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mja anayesibiwa na majonzi na huzuni na akasema:

اللهُمَّ إِني عَبْدُكَ وابنُ عَبْدِكَ وابْنُ أَمتِكَ نَاصيتي بيَدِكَ ماضٍ فِيَّ حُكْمُكَ عَدْلٌ فيَّ قَضَاؤُكَ أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ سَمَّيتَ بِهِ نَفْسَكَ أَوْ أَنْزَلْتَهُ في كِتَابِكَ أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحداً مِن خَلْقِكَ أَوِ اسْتَأْثَرْتَ بِه في علم الْغَيْبِ عِنْدَكَ أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ العظيمَ رَبيع قَلْبي ونورَ صَدْرِي وجلاءَ حُزْنِي وَذَهَابَ هَمِّي

“Ee Allaah! Hakika mimi ni mtumwa Wako, mtoto wa mtumwa Wako na mtoto wa mjakazi Wako. Utosi wangu uko mikononi Mwako. Yaliyopita kwangu yako katika hukumu Yako. Hukumu Yako ni adilifu kwangu. Nakuomba kwa kila Jina ambalo ni Lako ulilojiita Kwako mwenyewe au uliloliteremsha katika Kitabu Chako au ulilomfundisha yeyote katika viumbe Vyako au ulilolikhusisha Wewe mwenyewe katika elimu iliyojificha kwako, ujaalie Qur-aan tukufu iwe ni nguvu ya roho yangu na nuru ya kifua changu inayotoa huzuni wangu na kuondoka majonzi yangu”

isipokuwa Allaah humuondolea huzuni yake na dhiki yake na humbadilishia mahali pa huzuni hiyo kuwa furaha.”[7]

Ameipokea Ahmad katika “al-Musnad” na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh”.

[1] Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib” (98).

[2] at-Tirmidhiy (3436), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri na ngeni. Dhaifu mno kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (3436).

[3] Abu Daawuud (5049). Cheni yake ya wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib” (99) na Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Hibbaan (970).

[4] Abu Daawuud (1525), an-Nasaa’iy katika “´Amal-ul-Yawm wal-Laylah” (649) na Ibn Maajah (3882). Nzuri na pengine hata ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib” (100).

[5] an-Nasaa’iy katika “´Amal-ul-Yawm wal-Laylah” (650).

[6] at-Tirmidhiy (3505), an-Nasaa’iy katika “´Amal-ul-Yawm wal-Laylah” (656) na Ahmad (1/463-464). Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim, adh-Dhahabiy na al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib” (101).

[7] Ahmad (2/47), Ibn Hibbaan (972) na al-Haakim (1/509), aliyesema kuwa iko kwa mujibu wa sharti za Muslim. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Kalim at-Twayyib” (102).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 295-298
  • Imechapishwa: 08/09/2025