11- Saalim bin Abiyl-Ja´d al-Ashja´iy al-Ghatwafaaniy al-Kuufiy. Alikuwa ni Faqiyh na mwaninifu.

Amepokea kutoka kwa Thawbaan, mtumwa aliyeachwa huru na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Jaabir, Ibn ´Abbaas, an-Nu´maan bin Bashiyr, ´Abdullah bin ´Amr, Ibn ´Umar, Anas bin Maalik, baba yake Abul-Ja´d Raafiy´ na wengineo.

al-Hakam, Qataadah, Mansuur, al-A´mash. Husayn bin ´Abdir-Rahmaan na wengineo wamehadithia kutoka kwake.

Wamesema kuwa Abul-Ja´d alikuwa na wavulana sita. Wawili walikuwa Shiy´ah. Wawili walikuwa Murji-ah. Wawili walikuwa Khawaarij. Baba yao alikuwa akiwaambia:

“Allaah amekutenganisheni.”

Walikuwa wanaitwa ´Ubayd na ´Imraan, Ziyaad na Muslim na ´Abdullaah.[1]

12- Yahyaa amesema:

“Nilikuwa mimi na Abu Zakariyya nje ya mlango wa ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz na tukasikia kilio. Tukapata khabari kwamba kiongozi wa waumini amempa khiyari mke wake kati ya kuendelea kuishi nyumbani kwake na katika hali yake na kumjuza kwamba amekuwa mashghuli kutokamana na wanawake na kati ya kuhama kwenda nyumbani kwa baba yake. Ndio akalia na wajakazi wake nao wakalia.”[2]

13- Abu ´Ubaydah bin ´Uqbah bin Naafiy´ amesimulia kwamba aliingia kwa Faatwimah bint ´Abdil-Malik, mke wa ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz, na akasema:

“Si unieleze juu ya ´Umar?” Akasema: “Sijui kama alioga kutokamana na jimaa wala kuota tangu awe mtawala.”[3]

14- Abu ´Abdillaah ´Abdul-´Aziyz bin Rufay´ al-Asdiy at-Twaa-if al-Kuufiy. Alikuwa Muhaddith na mwaminifu.

Inasemekana ni mara chache alioa mwanamke isipokuwa mwanamke huyo aliomba talaka kutokana na wingi wa kufanya naye jimaa.”[4]

15- Zubayd bin al-Haarith al-Yaamiy al-Kuufiy. Haafidhw, mmoja katika wanachuoni wakubwa.

Ibn Shubrumah amesema:

“Zubayd alikuwa akiugawanya usiku wake sehemu tatu; sehemu juu yake mwenyewe, sehemu nyingine juu ya mwanae na sehemu nyingine juu ya mwanae mwingine ´Abdur-Rahmaan. Alikuwa kwanza anaswali sehemu yake.Kisha anamwamrisha mwanae wa kwanza aswali. Anapopatwa na uvivu basi anaswali sehemu yake iliyobaki. Halafu anamwamrisha mwanae mwingine aswali. Anapopatwa na uvivu basi anaswali sehemu yake iliyobaki. Hivyo basi anaswali usiku mzima.”[5]

16- Yuunus bin Muhammad al-Mu-aadib amesema kuwa Ziyaad amemweleza:

“Zubayd alikuwa ni mwadhini katika msikiti wake. Alikuwa akiwaambia watoto wadogo: “Njooni mswali, nitawapa njugu.” Wanaswali kisha wanamzunguka. Namuuliza juu ya hilo ambapo hujibu: “Kuna tatizo gani nikiwanunulia njugu kwa dirhamu tano ili waizowee swalah?”[6]

17- Ja´far bin Sulaymaan amesema:

“Muhammad bin al-Munkadir alikuwa akiweka shavu lake juu ya ardhi kisha akimwambia mama yake: “Simama uweke mguu wako juu ya shavu langu.”[7]

18- Ibn-ul-Munkadir amesema:

“Ndugu yangu ´Umar alikesha akiwa anaswali na mimi nimekesha nikiukumbatia mguu wa mama yangu. Sipendelei usiku wangu uwe kama wake.”[8]

19- ´Umar bin Shabiyb al-Musliy amesema:

“Baada ya Abu Ishaaq kuwa kipofu niliona namna Israaiyl anavyomwendesha na mwanae Yuusuf akimwelekeza.”[9]

20- ´Aliy bin al-Madiyniy amesema:

“Nduguye Suhayl [bin Abiy Swaalih] alifariki. Likampata jambo hilo kwelikweli mpaka akasahau Hadiyth nyingi.”[10]

[1] 5/109.

[2] 5/128.

[3] 5/135-136.

[4] 5/228.

[5] 5/296.

[6] 5/297.

[7] 5/356.

[8] 5/359.

[9] 5/399.

[10] 5/460.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Siyar A´laam-in-Nubalaa’
  • Imechapishwa: 25/01/2021