Ni ipi hukumu ya kumswalia maiti asiyekuwepo?

Ni ipi hukumu ya kumswalia maiti asiyekuwepo?

Swali: Ni ipi hukumu ya kumswalia maiti asiyekuwepo na kumswalia maiti aliye ndani ya kaburi? Je, hilo lina kikomo?

Jibu: Maoni sahihi ni kwamba kumswalia asiyekuwepo sio Sunnah. Isipokuwa tu kwa wale ambao hawakumswalia. Mfano wa hilo ni kama mtu amekufa kwenye bara au katika nchi ya kikafiri na haijulikani kama mtu huyo ameswaliwa. Katika hali hii kumswalia itakuwa ni wajibu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimswalia an-Najaashiy na akawaamrisha Maswahabah wake vilevile kumswalia ambapo akatoka nao kwenda pahala pa kuswalia na akawaswalisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[1].

Kumswalia asiyekuwepo ni suala ambalo halikuthibiti isipokuwa kwa anNajaashiy peke yake. Sababu ilikuwa haikutambulika kuwa aliswaliwa katika mji wake. Kuhusu wale waliojua kuwa maiti ameswaliwa katika mji wake sahihi ni kuwa haikusuniwa kumswalia.

Kuhusu kumswalia maiti aliyemo ndani ya kaburi ni Sunnah. Hilo limethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuna wanachuoni walioliwekea hilo kikomo cha mwezi mmoja na kuna wengine wasiyoonelea hivo. Sahihi ni kuwa hakuna kikomo. Lakini hata hivyo imeshurutishwa maiti ambaye anamswalia ndani ya kaburi awe amekufa katika uhai wa mswalaji huyu. Kwa msemo mwingine awe amekufa baada ya kuzaliwa kwake na hali ya kuwa ana uwezo wa kupambanua mambo. Iwapo atakufa kabla ya hapo itakuwa haikusuniwa kumswalia maiti huyu aliye ndani ya kaburi. Mfano wa hili mtu amekufa katika mwaka wa 1400 na akazaliwa mtu mwingine katika mwaka huo huo, haifai kwa mtoto huyu kumswalia maiti aliye ndani ya kaburi. Kwa kuwa alipokufa maiti mtoto huyu hakuwa miongoni mwa wanaotakiwa kuswali. Lakini iwapo atakufa mwaka 1400 na akaja mtu aliyazaliwa mwaka wa 1380, inafaa kwake kumswalia. Alipokufa maiti huyu mswalaji alikuwa miongoni mwa watu wanaotakiwa kuswali. Tumesema hivo ili asiwepo mtu atayezua Bid´ah ambapo akaenda kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na makaburi ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum), yaliyoko al-Baqiy´, swalah ya jeneza. Hili halikuthibiti.

Kwa ufupi ni kwamba amswalie maiti aliye ndani ya kaburi bila ya kuanisha muda ikiwa maiti huyo alikufa katika kipindi ambacho yule mswalaji ameshakuwa miongoni mwa watu wanaotakiwa kumswalia65.

[1] al-Bukhaariy (1333) na Muslim (62) na (951).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/146-147)
  • Imechapishwa: 15/09/2021