Ni ipi hukumu ya adhaana ya mnyoa ndevu, mvuta sigara na anayeburuza nguo yake?

ar-Raajihiy: Vipi ikiwa muadhini amenyoa ndevu?

Ibn Baaz: Hili ni jambo haliko dhahiri, huyo ni mwenye maasi ya wazi. Hiyo ni dhambi iliyo dhahiri. Tunamuomba Allaah atuepushe na hayo.

ar-Raajihiy: Je, asiadhini?

Jibu: Hawezi kuaminika katika uadhini wake. Inatakiwa kumteua mwingine badala yake, kwa sababu huyu si mtu mwenye heshima ya dini, bali ni mwenye maasi ya wazi.

Mwanafunzi: Je, mfungaji afungue kwa adhaana ya mnyoa ndevu ikiwa atasikia adhaana yake?

Ibn Baaz: Haaminiwi isipokuwa ikiwa ni adhaana ya mwingine au kama anajua kwa yakini kuwa jua limeshazama na wakati umeshaingia, basi hapo anaweza kufungua.

Mwanafunzi: Katika baadhi ya nchi waadhini ni watu walio wazi katika ufuska wao, kama wanyoa ndevu, wanavuta sigara na wanaovaa nguo chini ya vifundo vya miguu?

Ibn Baaz: Allaah awaongoe. Unatakiwa kuwaombea uongofu na kuwashauri na uwaambie viongozi wawabadilishe.

Mwanafunzi: Je, adhaana yao inatosheleza?

Ibn Baaz: Ni jambo linahitaji kuangaliwa vizuri. Isipokuwa ikiwa unajua kwamba wakati umeingia au wengien wameadhini. Ama katika dharurah, inaweza kusemwa kwamba kwa dharurah, kwa sababu balaa la kunyoa ndevu limeenea na baadhi yao wanaona kuwa ni jambo lisilokuwa na ubaya. Mtu anaweza kusema kwamba hapana vibaya wakati wa dharurah muda wa kuwa mtu huyo si mwenye kutuhumiwa uzembe katika adhaana yake. Hivyo katika dharurah anaweza kuaminiwa katika adhaana, swalah au kufungua. Lakini kadiri na inavyowezekana ni lazima kumwondoa na kuwaelekeza wahusika wamchague mtu mwingine. Hapana vibaya katika hali hiyo, kwa sababu dharurah zina hukumu zake. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) amesema:

وَمَا لَكُمْ أَلَّا تَأْكُلُوا مِمَّا ذُكِرَ اسْمُ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَقَدْ فَصَّلَ لَكُم مَّا حَرَّمَ عَلَيْكُمْ إِلَّا مَا اضْطُرِرْتُمْ إِلَيْهِ

”Kwani mna nini hata msile katika vile ambavyo vimetajiwa jina la Allaah na ilihali ameshapambanua kwenu yale Aliyokuharamishieni isipokuwa vile mlivyofikwa na dharura.”?[1]

Kwa hivyo inaweza kusemwa kwamba katika hali ya dharurah au kwa sababu ya kutokujua, adhaana yake inaweza kukubalika. Kwa sababu baadhi ya watu wanaona kunyoa ndevu au kuzikata kuwa ni jambo linaloruhusiwa na wanadanganywa na wale wanaodhaniwa kuwa ni wanazuoni na hivyo wakadanganyika na matokeo yake wakawafuata kichwa mchunga. Tunamuomba Allaah usalama.

[1] 06:119

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/31554/ما-حكم-اذان-حليق-اللحية-والمدخن-والمسبل
  • Imechapishwa: 05/11/2025