Swali: Allaah (´Azza wa Jall) kaniongoza baada ya kusikilia muhadhara wa mmoja katika wanachuoni kuhusu Aakhirah. Baada ya siku hii nilihisi utamu wa imani na tangu sasa naishi maisha mengine ya raha na mafanikio na raha na watoto wangu. Nawafunza Kitabu cha Allaah na kuwaita kwa Allaah na kumkumbuka Allaah katika hali zote.

Pia nilianza kuvaa mavazi ya Kiislamu ambayo yanaendana na mwanamke wa Kiislamu. Lakini pamoja na uzito wote huu na njia hii mpya nimeyochukua, familia yangu, ndugu zangu wote katika familia wananiona kama mgonjwa na ni mwenye wasiwasi. Ndio maana nimemtumia swali langu bwana muheshimiwa Shaykh Swaalih ili anifanye kubaki kwenye thabati na msimamo.

Jibu: Hii ni bishara ya kheri kwa mwanamke huyu ambaye aliathirika kwa muhadhara mzuri. Allaah amjaze aliyeutoa kheri. Namna hii yatakikana muhadhara kuwa, iwe ni wenye kuibainisha dini hii na kubainisha fadhila za dini hii na kuvutia watu kwayo. Muhadhara usizungumzia mambo mengine, kuingia kwenye siasa na mfano wa mambo kama hayo ambayo yanapoteza tu muda wa watu na linawaathiri na wala hawastafidi kitu. Bali wanadhurika. Namna hii unatakiwa kuwa mihadhara na khaswa khaswa kwenye misikiti. Khutbah za Ijumaa na mawaidha iwe namna hii. Ikumbushe Allaah (´Azza wa Jall), ikiwafunza watu wasioyajua katika mambo ya dini yao.

Na wewe mwanamke uliposema ya kwamba umetubu kwa Allaah na ukawa na msimamo katika dini ya Allaah na ukashikamana na Hijaab, jua kuwa hili ni kheri kwako na maisha yako ya sasa na si kama maisha yako ya kwanza. Maisha ya uongofu na imani. Ni juu yako kuwa na msimamo na kuendelea kwa hili. Jizidishie imani. Jizidishie kusikiliza mihadhara mizuri na Dhikr. Usibabaishwe na watu hawa waharibifu ambao wanataka kukurudisha nyuma na uache neema Aliyokupa nayo Allaah. Hawa ni katika Mashaytwaan wa kibinaadamu ambao wanapoteza watu na wanawakimbiza katika kheri.

Ni juu yako kushikama imara na dini yako na kuwa na subira kwa uliyomo. Ni juu yako kujifunza elimu yenye manufaa ili iwe kutubu kwako na ´Ibaadah zako zimejengeka juu ya elimu na juu ya elimu yenye manufaa.

  • Mhusika: ´Allaamah Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.sahab.net/forums/index.php?showtopic=133391
  • Imechapishwa: 17/09/2020