Inafaa kumswalia mtu aliyemuua mkewe na akajiua na yeye?

Swali: Aswaliwe mtu ambaye kamuua mkewe kisha na yeye akajiua?

Jibu: Ndio, aswaliwe. Kuua mtu hakumtoi katika Uislamu. Dalili ya kuwa hatoki katika Uislamu ni maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِصَاصُ فِي الْقَتْلَى ۖ الْحُرُّ بِالْحُرِّ وَالْعَبْدُ بِالْعَبْدِ وَالْأُنثَىٰ بِالْأُنثَىٰ ۚ فَمَنْ عُفِيَ لَهُ مِنْ أَخِيهِ شَيْءٌ فَاتِّبَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ وَأَدَاءٌ إِلَيْهِ بِإِحْسَانٍ ۗ ذَٰلِكَ تَخْفِيفٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَرَحْمَةٌ ۗ فَمَنِ اعْتَدَىٰ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَلَهُ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Enyi mlioamini! Mmeandikiwa [kulipiza] kisasi juu ya waliouawa; muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Anayesamehewa na nduguye kwa lolote basi kufuatilizwa kwake kuwe kwa wema na kumlipa kwake iwe kwa ihsani – hiyo ni takhafifu na huruma kutoka kwa Mola wenu. Na atayevuka mipaka baada ya hapo basi atapata adhabu iumizayo.”[1]

 Amefanya muuaji ni ndugu wa yule muuliwaji. Angelikuwa anatoka katika Uislamu basi asingelikuwa ni ndugu yake. Hata hivyo ni jambo la khatari hata kama hatoki katika Uislamu. Vilevile adhabu ni kali. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا

“Na yeyote atakayemuua muumini makusudi, basi malipo yake ni Moto ni mwenye kudumishwa humo na Allaah atamghadhibikia na atamlaani na atamuandalia adhabu kuu.”[2]

Kuna adhabu tano: Moto, kutiwa ndani yake kwa muda mrefu, Allaah amemghadhibikia, amemlaani na amemwandalia adhabu kubwa. Sio jambo rahisi. Lakini hata hivyo hatoki katika Uislamu. Aswaliwe na aombewe msamaha. Fadhila za Allaah ni pana.

[1] 02:178

[2] 04:93

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/150)
  • Imechapishwa: 15/09/2021