Anaogopa muda wa swalah kuisha ikiwa ataoga

Swali: Vipi ikiwa mtu atachelea muda wa swalah kumalizika kwa sababu ya kuoga josho kubwa?

Jibu: Ikiwa alikuwa macho na akazembea, basi aoge na kuswali. Lakini kama alikuwa amelala, hapana vibaya hata kama muda wa swalah umepita. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipolala akakosa swalah, aliichelewesha mpaka walipoamka. Baada ya hapo wakatawadha na kuswali, kwani alikuwa na udhuru. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kupitikiwa na usingizi au akaisahau swalah, basi aiswali pale atapoikumbuka. Haina kafara nyingine isipokuwa hiyo.”[1]

Lakini mtu akiwa macho, haifai kwake kuchelewesha swalah. Anatakiwa aswali katika wakati wake kulingana na hali yake.

´Allaamah ar-Raajihiy: Vipi akiwa macho na akaichelewesha swalah?

Ibn Baaz: Haijuzu kwake kuchelewesha. Aliye macho anapaswa kuswali ndani ya muda wake.

´Allaamah ar-Raajihiy: Vipi ikiwa ameichelewesha na anaogopa muda wa swalah kumalizika iwapo ataoga?

Ibn Baaz: Dhahiri ni kwamba katika hali hiyo aswali kwa kufanya Tayammum na asicheleweshe. Ikiwa kutafuta maji ya wudhuu´ au kuoga kutasababisha muda wa swalah kuisha. Isipokuwa ikiwa alikuwa amelala, basi ana udhuru hata kama muda wa swalah umepita, kwa sababu aliyelala au kusahau hana kosa.

[1]al-Bukhaariy (597) na Muslim (684).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/31543/ما-حكم-من-خشي-خروج-الوقت-اذا-اغتسل
  • Imechapishwa: 04/11/2025