1 – Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kumbukeni kwa wingi kile kinachokata ladha – kifo.”

2 – Mbali na zile busara zote tulizotaja katika kitabu chetu hichi ni wajibu kwa mwenye busara daima kukumbuka kifo katika nyakati zote na asighurike na maisha haya ya dunia. Kifo ni kinu ambacho mabaya yake huzunguka kati ya viumbe wote. Kifo ni chombo ambacho ni lazima kwa kila chenye roho anywe kutoka ndani yake na akionje.

3 – Kifo kinakata ladha. Kinazamisha matamanio. Kinachafua nyakati. Kinasambaratisha kasoro.

4 – Abul-´Ataahiyah amesema:

“Niliingia kwa kiongozi wa waumini Haaruun [ar-Rashiyd]. Aliponiona akasema: “Abul-´Ataahiyah?” Nikasema: “Abul-´Ataahiyah.” Akasema: “Mshairi?” Nikasema: “Mshairi.” Akasema: “Niwaidhi kwa mashairi mafupi.” Ndipo nikamsomea:

Usihisi salama kwa kifo

ijapo utakuwa umejilinda na walinzi

Unapasa kutambua kwamba mishale ya kifo ni yenye kumlenga

Kila mwenye kujilinda na silaha na ngao

Unatarajia kuokoka na hutaki kufata njia zake?

Mashua haipiti nchi kavu

Haaruun akaanguka chini hali ya kuzimia.”

5 – Mwenye busara hasau kitu kinachomsubiri. Ni ummah ngapi zimetokomezwa na kifo? Ni miji mingapi imesambaratishwa na kifo? Ni wanawake wangepi wamefanywa wajane? Ni watoto wangapi wamefanywa kuwa mayatima? Ni ndugu wangepi wamebakiwa wenyewe?

6 – Mwenye busara haghuriki na hali ambayo mwisho wake unapelekea katika yale tuliyoyataja. Hategemei katika maisha ambayo yanaishilia kwa njia ile tuliyoitaja. Hasahau ile hali ambayo ni lazima itamfika. Kifo ni muwindaji ambaye haswindwi na mwenyeji wala mkimbizi hamtoroki.

7 – Ibn-us-Simaak amesema:

“Hapo kale alikuweko mvuvi mmoja ambaye alitoka kwenda kuvua samaki. Baada ya kutupa wavu ndani ya bahari tahamaki akavuta fuvu la binadamu. Akawa analitazama, analia na kusema: “Ulikuwa mtukufu, lakini hukuachwa kwa sababu ya utukufu wako. Ulikuwa tajiri, lakini hukuachwa kwa sababu ya utajiri wako. Ulikuwa fakiri, lakini hukuachwa kwa sababu ya ufukara wako. Ulikuwa mkarimu, lakini hukuachwa kwa sababu ya ukarimu wako. Ulikuwa mshupavu, lakini hukuachwa kwa sababu ya ushupavu wako. Ulikuwa mjuzi, lakini hukuachwa kwa sababu ya ujuzi wako.” Akawa anayarudirudi maneno haya na huku analia.

8 – ´Abdul-Man´im ar-Rayyaahiy amesema:

“Siku moja alipotea Maalik bin Diynaar. Aliporudi wakamuuliza ni wapi alipokuwa. Akasema kwamba alitoka kwenda “al-Ubullah.” Wakamuuliza ni yapi mazuri aliyoyaona. Akasema: “Nilimwona mwanamke mmoja akiswali.” Wakamuuliza ni kipi cha ajabu alichokiona. Akasema: “Kasiri huko Bahrain. Juu ya mlango wake kulikuwa kumeandikwa:

Nataka kuwa na maisha kama wale wenye furaha zaidi

Niliishi maisha ya kupendeza na ya furaha

Naapa kwa Mola wa watu kwamba hakukuwa na ucheleweshaji

Kabla ya mimi kuachana na jamaa na marafiki

9 – Swaalih al-Murriy amesema:

“Siku moja wakati ambapo kulikuwa na joto kali niliingia makaburini. Nikayatazama makaburi yalivotulia. Utasema ni watu walionyamaza kimya. Nikasema: “Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu! Ni nani atakayekusanya roho na miili yenu baada ya kutengana kwake? Ni nani atakayekuhuisheni baada ya kuteketea?” Ndipo kukasikika sauti kutoka katika moja ya mashimo: “Ee Swaalih!

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ ۚ ثُمَّ إِذَا دَعَاكُمْ دَعْوَةً مِّنَ الْأَرْضِ إِذَا أَنتُمْ تَخْرُجُونَ

“Miongoni mwa ishara Zake, ni kwamba mbingu na ardhi zimesimama kwa amri Yake kisha atakapokuiteni wito mmoja, tahamaki mtatoka ardhini.”[1]

Naapa kwa Allaah nikaanguka hali ya kuzimia.

10 – Nimeyataja machache, kutokamana na mengi mno, katika mapokezi katika kitabu hiki. Natumai yanatosha kwa yule anayetaka kufuata njia ya wenye busara, akiyazingatia na kuyatendea kazi.

Swalah na salamu zimwendee Nabii wa mwisho Muhammad na kizazi chake kisafi. Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] 30:25

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 283-289
  • Imechapishwa: 14/09/2021