Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

التحيات لله

maadhimisho yote yanamstahiki Allaah kwa njia inayolingana na Ukubwa na Utukufu Wake, kama Rukuu´, Sujuud na kudumu milele. Vyote ambavyo Mola wa walimwengu huadhimishwa kwavyo, vinamstahiki Allaah. Atakayemfanyia katika hayo chochote asiyekuwa Allaah ni mshirikina kafiri.

MAELEZO

Kuinama hakukuwi isipokuwa kwa Allaah. Kwa sababu ndani yake kuna maadhimisho. Rukuu´ haiwi isipokuwa kwa Allaah. Sujuud haiwi isipokuwa kwa ajili ya Allaah.

Haijuzu kumuinamia mtu wakati wa kumswalia. Kuinama ni kuadhimisha. Maadhimisho yanakuwa kwa Allaah (Subhaanah) pekee. Vilevile haijuzu kumfanyia Rukuu´ na Sujuud mtu. Matendo haya ni ´ibaadah anayofanyiwa Allaah pekee.

Maneno yake:

“Kudumu milele.”

Hakukuwi isipokuwa kwa Allaah. Kuhusu viumbe watamalizika na kuteketea. Amesema (Ta´ala):

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ

“Kila aliyekuwa juu yake [ardhi] ni mwenye kutoweka.”[1]

Yeyote mwenye kuona kuwa kuna yeyote atakayebaki na kudumu milele mbali na Allaah ni kafiri. Kubaki na kudumu milele ni kwa Allaah pekee. Viumbe watateketea na kumalizika. Hakuna atakayebaki isipokuwa vile ambavo Allaah ameviandikia kubaki kama mfano wa ´Arshiy, Kursiy, Pepo, Moto na kifupa kilicho kwenye uti wa mgongo wa mtu. Roho zinapotoka haziteketei bali zinabaki ima ndani ya neema au adhabu. Vilevile Ubao uliohifadhiwa na kalamu:

Vitu nane ni vyenye hukumu ya kubaki yenye kuvienea

Viumbe vyengine vilivyobaki ni vyenye kuangamia

´Arshiy, Kursiy, Moto, Pepo, kifupa, roho na pia Ubao na kalamu

Maneno yake mtunzi:

“Atakayemfanyia katika hayo chochote asiyekuwa Allaah ni mshirikina kafiri.”

Kama ambaye anamfanyia Rukuu´ asiyekuwa Allaah hali ya kumwabudu, anayemsujudia asiyekuwa Allaah, anayemtukuza asiyekuwa Allaah katika yale mambo ambayo ni maalum kufanyiwa Allaah na kadhalika.

[1] 55:26

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 95-96
  • Imechapishwa: 28/06/2022