Uombezi mbele ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) umethibiti katika Qur-aan na Sunnah. Hilo ni kwa njia ya kwamba Allaah atawakirimu baadhi ya waja Wake wawaombee ndugu zao wasalimike kutokamana na adhabu siku ya Qiyaamah. Yote hayo kwa ajili ya kumkirimu yule mwombezi na rehema kwa mwenye kuombewa. Huu ndio uombezi mbele ya Allaah. Allaah atawapa idhini baadhi ya mawalii Wake wamuombe Allaah awasamehe wale ambao walikuwa wanastahiki adhabu. Ni jambo limethibiti katika Qur-aan. Lakini hata hivyo kwa sharti:

Ya kwanza: Uombezi huo uombwe kutoka kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) na Allaah aidhinishe. Hakuna yeyote awezaye kuomba mbele ya Allaah isipokuwa kwa idhini Yake. Tofauti na viumbe. Waombezi wanaweza kuomba mbele yao ingawa hawakutoa idhini. Bali huenda hata wakachukia hilo. Ama Allaah (Jalla wa ´Alaa) hakuna yeyote awezaye kushufai isipokuwa kwa idhini Yake:

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?”[1]

Ya pili: Mwombewaji awe miongoni mwa waumini pamoja na kwamba yuko na mambo yanayomfanya kustahiki kuadhibiwa kutokana na dhambi yake kubwa aliyoifanya. Ni miongoni mwa waumini na miongoni mwa waliofanya dhambi kubwa zilizo chini ya shirki. Kuhusu mshirikina Allaah hayuko radhi aombewe na hakubali uombezi juu yake. Amesema (Ta´ala):

مَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ حَمِيمٍ وَلَا شَفِيعٍ يُطَاعُ

”Madhalimu hawatokuwa na rafiki wa dhati na wala mwombezi anayetiiwa.”[2]

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“… na wala hawataomba uombezi wowote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.”[3]

Allaah aridhie maneno na matendo yake na awe ni muumini. Ama kafiri Allaah hamridhii. Uombezi hautomfaa kitu. Amesema (Ta´ala):

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi haitowafaa uombezi wowote wa waombezi.”[4]

Zikitimia sharti mbili ndipo Allaah atampa idhini mwombezi aombee na amridhie mwombewaji. Uombezi ni haki. Ikikosekana sharti moja uombezi unarudishwa. Amesema (Ta´ala):

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ

”Malaika wangapi mbinguni haitowafaa kitu chochote uombezi wao isipokuwa baada ya kuwa Allaah ametolea idhini kwa amtakaye… ”

Hii ni sharti ya kwanza.

وَيَرْضَىٰ

“… na akaridhia.”[5]

Hii ni sharti ya pili.

Huu ndio uombezi mbele ya Allaah. Unafaa kwa sharti mbili. Zikitimia sharti hizi mbili uombezi ni sahihi na ni wenye kukubalika mbele ya Allaah (´Azza wa Jall). Ikikosekana sharti moja wapo ni wenye kurudishwa na haukubaliwi.

[1] 02:255

[2] 40:18

[3] 21:28

[4] 74:48

[5] 53:26

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 82-84
  • Imechapishwa: 09/04/2021