49. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya hali nzito siku ya Qiyaamah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Roho kurudishwa kwenye viwiliwili na watu wasimame mbele ya Mola wa walimwengu hali ya kuwa ni miguu peku, uchi na pasi na kutahiriwa. Jua litasogezwa karibu nao.”

MAELEZO

Baada ya kaburi ni kufufuliwa. Roho zitarudishwa kwenye viwiliwili. Washirikina na wakanamungu wamepinga jambo hilo. Tumekwishataja baadhi ya dalili kuonyesha kuwa jambo hilo limethibiti ndani ya Qur-aan tukufu. Nazo ni dalili za kiakili zilizotajwa ndani ya Qur-aan kama mfano:

1- Ambaye ameweza kukianza kitu ana haki zaidi ya kuweza kukirudi. Hii ni dalili ya kiakili na ipo dalili ya kinukuu pia.

2- Ambaye ni muweza wa kuihuisha ardhi baada ya kufa kwake ni muweza wa kuihuisha miili baada ya kufa kwake.

3- Allaah (Subhaanah) ametakasika kutokamana na mchezo na dhuluma. Ni lazima atekeleze uadilifu kati ya waja Wake, jambo ambalo litakuwa Aakhirah na haliwi duniani. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema kuhusu kusimama kutoka ndani ya makaburi:

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ

“Itapulizwa katika baragumu, basi watazimia wale walioko mbinguni na ardhini… “[1]

Kuzimia bi maana kufa. Hili ni baragumu ya kuzimia. Atazimia kila aliyeko mbinguni na ardhini isipokuwa wale atakao Allaah. Imesemekana kuwa ni Malaika. Kuna maoni mengine vilevile yamesema kuwa ni al-Huur al-´Ayn.

Kisha ataamrisha kutapulizwa baragumu la pili ambapo watu watasimama kutoka ndani ya makaburi yao kumwendea Mola wa walimwengu. Katika baragumu la pili ndipo roho zitaruka kwenda katika viwiliwili vyake. Ardhi itawapasukia:

يَوْمَ تَشَقَّقُ الْأَرْضُ عَنْهُمْ سِرَاعًا

”Siku itakayowapasukia ardhi  [watoke] upesiupesi.”[2]

Watatoka ndani ya makaburi yao na waharakishe kwenda katika uwanja wa hesabu kana kwamba ni nzige zilizotawanyika:

فَتَوَلَّ عَنْهُمْ ۘ يَوْمَ يَدْعُ الدَّاعِ إِلَىٰ شَيْءٍ نُّكُرٍ خُشَّعًا أَبْصَارُهُمْ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ

“Basi jitenge nao. Siku atakayoita mwitaji kuliendea jambo baya mno la kuogofya. Macho yao yakiwa dhalili, watatoka ndani ya makaburi… “

Bi maana kutoka ndani ya makaburi yao:

الْأَجْدَاثِ كَأَنَّهُمْ جَرَادٌ مُّنتَشِرٌ

“… kama kwamba wao ni nzige waliosambaa.”[3]

Wataifunika ardhi kutokana na wingi wao:

مُّهْطِعِينَ إِلَى الدَّاعِ

“Wenye kukimbia mbio huku wakibenua shingo zao wakielekea kwa mwitaji.”[4]

Wanyenyekevu hakuna yeyote mwenye kuchelewa nyuma; si kafiri wala muislamu. Hakuna yeyote katika wao atakayechelewa nyuma wala hakuna yeyote awezaye kufanya hivo. Katika Aayah nyingine imekuja:

يَوْمَ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ سِرَاعًا كَأَنَّهُمْ إِلَىٰ نُصُبٍ يُوفِضُونَ

”Siku watapotoka makaburini upesiupesi kama kwamba wanakimbilia golini.”[5]

Golini ni mahali watatoka waharakishe. Wataandamwa na Malaika na hakuna yeyote awezaye kukwepa.

Pindi Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) atapotaka kuwafufua watu kutoka ndani ya makaburi yao atatuma aina fulani ya mvua itayoteremkia kutoka juu na haitozuiwa na kitu; si paa wala kitu kingine. Itaanguka chini kwenye ardhi na itafika mpaka kwenye viwiliwili ndani ya makaburi. Watakua kama unavyokuwa mmea na miili itajengeka kama ilivyokuwa hapo kabla:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ ۚ ثُمَّ إِذَا دَعَاكُمْ دَعْوَةً مِّنَ الْأَرْضِ إِذَا أَنتُمْ تَخْرُجُونَ

“Miongoni mwa alama Zake, ni kwamba mbingu na ardhi zimesimama kwa amri Yake kisha atakapokuiteni wito mmoja, tahamaki mtatoka ardhini.”[6]

وَاسْتَمِعْ يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ

”Sikiliza Siku atakayonadi mwenye kunadi kutoka mahali pa karibu.”[7]

Atanadi mwenye kunadi akisema:

“Enyi mifupa mliyokwishaoza, nyama zilizokwishateketea na hisia zenye kutawanyika! Hakika Allaah anakuamrisheni mkusanyike kwa ajili ya kuhukumiwa.”[8]

Ndipo watu watakusanyika kutoka chini ya udongo. Mwili wake utakusanyika kama ulivyokuwa isipokuwa tu utakuwa hauna roho kiasi cha kwamba akipitiwa na mtu aliyekuwa anamjua duniani atasema: “Huyu ni fulani. Hakuna kitu kitachombadilika.”

Kisha ataamrishwa Israafiyl apulize baragumu na roho ziruke. Kwa sababu roho zitakuwa zimekusanyika ndani ya lile baragumu. Kila roho itaingia kwenye ndani ya mwili wake. Kisha wahuishwe na waamrishwe katika uwanja. Watasimama kutoka ndani ya makaburi yao na waharakishe kwenda katika uwanja kisha wakusanyike hapo. Watasimama kwa miguu yao katika shida, dhiki, joto kali, jua litasogezwa karibu na vichwa vyao, wapigwe na jasho na msongamano mkubwa. Kwa sababu wa mwanzo wao na wa mwisho wao watakusanyika katika uwanja mmoja. Watakusanyika na watahisi jasho kali.  Wanatofautiana katika jasho; wako miongoni mwao ambao lile jasho litawafunika, wengine litawafunika mpaka nusu ya mwili wao, wengine litawafunika mpaka kwenye magoti yao na kadhalika.

Kusimama kutakuwa kwa miaka elfu khamsini. Watakuwa ni wenye kodoa macho yao, miguu peku, hawana mavazi na wakiwa bila kutahiriwa. Watasimama katika uwanja huu kisimamo hichi kirefu ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) atawakusanya wa mwanzao wao na wa mwisho wao.

[1] 39:68

[2] 50:44

[3] 54:06-07

[4] 54:08

[5] 70:43

[6] 30:25

[7] 50:41

[8] Tazama ”Tafsiyr-ut-Twabariy” (26/183).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 72-74
  • Imechapishwa: 07/04/2021