Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

171 – Uko kati ya kuchupa mipaka na kuzembea, kufananisha na kukanusha, utenzwaji nguvu na makadirio, usalama na kukata tamaa.

MAELEZO

Uislamu uko kati ya kuchupa mipaka na kuzembea. Uislamu uko kati na kati, hakuna ususuwavu wala uzembe. Ukatikati ndio bora. Ndio maana Allaah (Subhaanah) akasema:

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ غَيْرَ الْحَقِّ

“Sema: “Enyi watu wa Kitabu! Msichupe mipaka katika dini yenu bila ya haki.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wameangamia wanaojikakama. Wameangamia wanaojikakama. Wameangamia wanaojikakama.”[2]

Wanaojikakama ni wale wanaochupa mipaka katika mambo ya dini. Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Watu watatu walikuja kwa wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwauliza kuhusu ´ibaadah zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walipoelezwa ni kana kwamba walizidogesha na wakasema: “Wapi kwa wapi sisi na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Kwani Allaah amemsamehe madhambi yake yaliyotangulia na yanayokuja huko mbele.” Mmoja wao akasema: “Mimi daima nitaswali usiku.” Mwingine akasema: “Mimi nitafunga mwaka mzima na sintofungua.” Mwingine akasema: “Mimi najitenga na wanawake na kamwe sintooa.” Ndipo akaja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Nyinyi ndio ambao mmesema kadhaa na kadhaa? Naapa kwa Allaah! Mimi namuogopa na namcha Allaah zaidi kuliko nyinyi, lakini nafunga na nala, naswali na nalala, na nawaoa wanawake. Hivyo basi, yule atakayeenda kinyume na Sunnah zangu basi si katika mimi.”[3]

Kwa sababu huku ni kuchupa mpaka yale ambayo Allaah ameamrisha. Allaah (Subhaanah) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُحَرِّمُوا طَيِّبَاتِ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكُمْ

“Enyi mlioamini! Msiharamishe vizuri Aliyokuhalalishieni Allaah… “[4]

Msifanye hivo kwa njia ya dini. Baada ya hapo akasema (Subhaanah):

وَلَا تَعْتَدُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُعْتَدِينَ

”… na wala msipindukie mipaka. Hakika Allaah hawapendi wachupao mipaka.”[5]

Aayah inakaripia pande zote mbili. Dini ni kati na kati.

[1] 5:77

[2] Muslim (2670).

[3] al-Bukhaariy (5063) na Muslim (1052).

[4] 5:87

[5] 5:87

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 258-259
  • Imechapishwa: 07/05/2025