Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

162 – Yule mwenye kuwazungumzia vizuri Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakeze waliosafishwa na kila najisi na kizazi chake waliotakaswa na kila uchafu, basi huyo amesalimika kutokana na unafiki.

MAELEZO

Baada ya kumaliza kutaja yale yanayopasa juu ya Maswahabah, ndipo akaanza kutaja watu wa nyumbani kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wa mwanzo wanaoingia katika watu wa familia yake ni wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا

”Hakika si venginevyo Allaah anataka akuondosheeni maovu, enyi watu wa nyumbani kwa Mtume, na akutakaseni mtakaso barabara.”[1]

Hapa wanazungumzishwa wao. Wa mwanzo wanaoingia katika watu wa nyumbani kwake ni wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kisha jamaa zake ambao ni familia ya al-´Abbaas, familia ya Abu Twaalib, familia ya al-Haarith bin ´Abdil-Muttwalib.

Raafidhwah wanamtukana ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) na wanamtuhumu kwa mambo ambayo Allaah amemtakasa nayo. Huku ni kumkadhibisha Allaah (´Azza wa Jall) na ni kumtuhumu kuwa alimchagulia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwanamke asiyemfaa, jambo ambalo ni kumkufuru Allaah. Amesema (Ta´ala):

الْخَبِيثَاتُ لِلْخَبِيثِينَ وَالْخَبِيثُونَ لِلْخَبِيثَاتِ ۖ وَالطَّيِّبَاتُ لِلطَّيِّبِينَ وَالطَّيِّبُونَ لِلطَّيِّبَاتِ

“Maneno maovu ni kwa ajili ya watu waovu na watu waovu kwa maneno maovu, na maneno mema ni kwa ajili ya watu wema, na watu wema kwa maneno maovu.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mzuri – Allaah hawezi kumchagulia isipokuwa wanawake wazuri.

Dhuriya yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanaokusudiwa ni watoto zake, watoto wa msichana wake Faatwimah, nao ni al-Hasan na al-Husayn, na watoto wao. Hiki ndio kizazi chake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1]33:33

[2]24:26

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 235
  • Imechapishwa: 28/04/2025