13. Matendo yote ya mshirikina ni yenye kuporomoka

Kafiri hana uombezi. Hainufaishi kitu kuamini  kwake kwamba hawa ni mawalii na kwamba wana jaha. Jaha ni ya kwao na matendo mema ni ya kwao. Hayamnufaishi kitu haya anayotegemea. Kadhalika Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) matendo ni ya kwao, wema ni wa kwao. Mambo hayo hayatomfaa kitu mshirikina ambaye anaamini kwamba ni waja wema, kwamba ni mawalii na kwamba wao ni Mitume kutokana na shirki iliyobomoa matendo yake na kule kuwaomba kwao badala ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.”[1]

Mshirikina matendo yake ni yenye kuporomoka. Ni mamoja amemshirikisha Mtume, walii, nyota, jini au sanamu. Matendo yake ni yenye kuporomoka na kuharibika. Kuwategema kwao kwa sababu eti ni mawalii na ni Mitume ni mambo ya batili. Ni kweli kwamba wao ni mawalii na ni Mitume. Lakini hata hivyo haifai kufungamana nao kama ambavyo haifai kuwategemea Malaika, majini, masanamu, nyota na vyenginevyo. Yote haya yako wazi kwa waumini na wanachuoni. Lakini yanaweza kuwa ni yenye kufichikana kwa baadhi ya watu kwa sababu ya uchache wa elimu na kutokuwa na ujuzi. Baadhi ya mambo yanaweza kuwababaisha. Lakini inakupasa wewe kujifunza. Kwani hili ni jibu zuri. Mweleze kwamba unataka kumwambia kitu cha wazi na mpe dalili ilio wazi na kwamba nyote wawili achaneni na kitu chenye kuwatatiza. Mweleze kwamba Allaah amesema kuwa wapotofu ndio hufuata yale maandiko yasiyokuwa wazi. Hivyo nyote wawili muachane na yasiyokuwa wazi na kwamba mfuate maandiko yaliyo wazi pale alipobainisha (Ta´ala) katika maneno Yake:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Wanaabudu badala ya Allaah ambavyo haviwadhuru wala haviwanufaishi na huku wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[2]

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Wale waliojichukulia badala Yake walinzi [wakisema:] “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie.”[3]

Haya ni mambo yako wazi aliyoyabainisha wakati alipokuwa anawaraddi:

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine – hana ushahidi wa wazi juu ya hilo – basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake. Hakika hawafaulu makafiri.”[4]

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[5]

فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ

“Basi mwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini.”[6]

Zipo dalili zengine mbali na hizi.

[1] 06:88

[2] 10:18

[3] 39:03

[4] 23:117

[5] 72:18

[6] 39:02

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 38-39
  • Imechapishwa: 14/10/2021