Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

89 – Akayakadiria yote hayo makadirio ya kukata na hakuna awezaye kuyachengua, kupingana nayo, kuyaondoa, kuyageuza, kuyapunguza wala kuyaongeza katika viumbe Wake katika mbinguna ardhiZake.

MAELEZO

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameyajua na akayakadiria:

وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا

”Ameumba kila kitu kisha akakikadiria kipimo sawasawa.”[1]

Mambo hayawi kwa vurugu wala pasi na mpangilio. Yote yamepangwa na kudhibitiwa kwa mipango, makadirio na uandishi wa Allaah. Allaah ametakasika kutokamana na vurugu na upuuzi. Hakuna yeyote awezaye kubadilisha yale aliyoyapanga Allaah na kuyakadiria. Hakuna awezaye kurudisha wala kupingana na hukumu Yake:

وَاللَّـهُ يَحْكُمُ لَا مُعَقِّبَ لِحُكْمِهِ ۚ وَهُوَ سَرِيعُ الْحِسَابِ

“Allaah anahukumu na hakuna wa kupinga hukumu Yake; Naye ni Mwepesi wa kuhesabu.”[2]

Hakuna yeyote awezaye kutengua wala kuzidisha chochote katika makadirio ya Allaah. Makadirio ni kitu kimeshahukumiwa na kumalizwa.

Pindi muislamu atakapoyaamini haya basi ataepuka mashaka na misononeko mingi. Lakini hiyo haina maana kuwa ategemee makadirio na akaacha kufanya matendo. Inapokuja katika matendo ameamrishwa kufanya matendo, kutafuta riziki na kufanya sababu. Inapokuja katika matokeo ni jambo liko mikononi mwa Allaah (´Azza wa Jall).

[1]25:2

[2] 13:41

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 120-121
  • Imechapishwa: 06/11/2024