10. Maadui wa Mitume na wafuasi wao katika njia ya haki

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na jua kwamba Allaah (Subhaanah) kwa Hekima Yake hakutuma Mtume yeyote kwa Tawhiyd hii isipokuwa alimuwekea maadui, kama alivyosema (Ta´ala):

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا

“Vivyo hivo tumemfanyia kila Nabii maadui mashaytwaan wa kiwatu na kijini – wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupambapamba  – kwa udanganyifu.” (al-An´aam 06 : 112)

Na yawezekana maadui wa Tawhiyd wakawa na elimu kubwa, vitabu na hoja. Kama alivyosema (Ta´ala):

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَرِحُوا بِمَا عِندَهُم مِّنَ الْعِلْمِ

”Basi ilipowajia Mitume yao kwa hoja za wazi, walifurahia kwa yale waliyokuwa nayo katika elimu.” (al-Ghaafir 40 : 83)

Ukishajua hilo, na ukajua ya kwamba ni lazima wawepo maadui ambao wamekaa katika njia ya Allaah, ni watu wenye ufaswaha, elimu na hoja, basi lililo la wajibu kwako ni kujifunza kutoka katika dini ya Allaah kile ambacho itakuwa ni silaha yako ili kuweza kupambana na mashaytwaan hawa ambao kasema kiongozi wao kumwambia Mola Wako (´Azza wa Jall):

لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

”Nitawakalia katika njia Yako iliyonyooka. Kisha nitawaendea mbele yao na nyuma na kuliani kwao na kushotoni kwao na wala hutopata wengi wao ni wenye kushukuru.” (al-A´raaf 07 : 16-17)

Lakini ukimuelekea Allaah (Ta´ala) na ukasikiliza hoja Zake na ubainisho Wake, hutokhofu na wala hutohuzunika.

إِنَّ كَيْدَ الشَّيْطَانِ كَانَ ضَعِيفًا

”Hakika hila za shaytwaan ni dhaifu.” (an-Nisaa´ 04 : 76)

Mtu ambaye si msomi katika wapwekeshaji anashinda watu elfu katika wanachuoni wa washirikina hawa. Kama alivyosema (Ta´ala):

وَإِنَّ جُندَنَا لَهُمُ الْغَالِبُونَ

”Hakika jeshi Letu ndilo litakaloshinda.” (asw-Swaaffaat 37 : 173)

Jeshi la Allaah ndio washindi kwa hoja na kwa ulimi, kama ambavyo wanashinda kwa panga na kwa mikuki. Hata hivyo khofu iko kwa yule mpwekeshaji ambaye anapita katika njia bila ya kuwa na silaha. Allaah (Ta´ala) ametuneemesha kwa Kitabu Chake ambacho amekifanya ni chenye kubainisha kila kitu na ni uongofu, rehema na bishara njema kwa Waislamu. Mtu wa batili hawezi kuja na hoja isipokuwa katika Qur-aan kuna yanayoivunja na kubainisha ubatilifu wake. Kama alivyosema (Ta´ala):

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا

“Wala hawakujii kwa mfano wowote isipokuwa Tunakuletea haki na tafsiri bora kabisa.” (al-Furqaan 25 : 33)

Wamesema baadhi ya wafasiri, Aayah hii ni jumla kwa kila hoja ambayo watakuja nayo watu wa batili mpaka siku ya Qiyaamah.

MAELEZO

Na jua kwamba… – Tokea wakati wa Nuuh mpaka wakati wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam). Haya ni kwa sababu ya majaribio na mtihani. Anawajaribu wema kwa kuwatumia waovu. Anawajaribu Mitume kwa maadui. Anawajaribu wanaolingania kwa Allaah kwa maadui zao. Hivyo ni lazima kujiandaa na kubeba silaha kwa ajili ya kupambana na watu hawa. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا ۚ وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ مَا فَعَلُوهُ ۖ فَذَرْهُمْ وَمَا يَفْتَرُونَ

“Vivyo hivo tumemfanyia kila Nabii maadui mashaytwaan wa kiwatu na kijini – wakifundishana wao kwa wao maneno ya kupambapamba  – kwa udanganyifu. Lau angetaka Mola wako, basi wasingeliyafanya hayo. Hivyo basi waachilie mbali na wanayoyazua!”

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِّنَ الْمُجْرِمِينَ ۗ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ هَادِيًا وَنَصِيرًا

“Na hivyo ndivyo Tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wahalifu. Na Mola wako Anatosheleza kuwa ni Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru.”[1]

Mitume wana maadui ambao wana shubuha na hoja wanazozitumia dhidi ya Mitume na wafuasi wao. Wana vitabu wanavyorejelea na kutaka kuwababaisha watu kwavyo. Amesema (Ta´ala):

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَرِحُوا بِمَا عِندَهُم مِّنَ الْعِلْمِ

”Basi ilipowajia Mitume yao kwa hoja za wazi, walifurahia kwa yale waliyokuwa nayo katika elimu.”

Bi maana elimu batili. Ni elimu isiyokuwa na manufaa. Lakini wanaitumia kutaka kuwababaisha wale walinganizi wa uongofu na Mitume. Lakini midhali mtu wa haki atakuwa juu ya haki na ubainifu basi hatobabaishwa na shubuha zao. Bali atazipondaponda na atabainisha ubatilifu wake. Kwa sababu yuko juu ya elimu. Amesema (Ta´ala):

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ

”Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah kwa ujuzi.”[2]

Kama ambavyo Mitume walizipondaponda na wakabainisha ubatilifu wake, kadhalika wafuasi wa Mitume ambao wanabainisha na kusambaratisha hoja za watu wa batili, utata wao, wanafichua upindaji wake, wanawawekea watu haki wazi kutokana na ile elimu na dalili za Shari´ah walizopewa na Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا

“Wala hawakujii kwa mfano wowote isipokuwa Tunakuletea haki na tafsiri bora kabisa.”[3]

وَلَقَدْ سَبَقَتْ كَلِمَتُنَا لِعِبَادِنَا الْمُرْسَلِينَ إِنَّهُمْ لَهُمُ الْمَنصُورُونَ وَإِنَّ جُندَنَا لَهُمُ الْغَالِبُونَ

“Hakika limekwishatangulia neno Letu kwa waja Wetu Mitume wetu kwamba: “Hakika wao bila shaka ndio wenye kunusuriwa na kwamba hakika jeshi Letu ndilo litakaloshinda.”[4]

وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ

“Bila shaka Allaah atamnusuru yule mwenye kuinusuru dini Yake – hakika Allaah ni Mwenye nguvu asiyeshindikana – ambao Tukiwamakinisha katika ardhi husimamisha swalah na hutoa zakaah na huamrisha mema na hukataza maovu.”[5]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ

“Enyi mloamini! Mkisaidia kuinusuru dini ya Allaah, basi Atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu.”[6]

Mtu ambaye ana ujuzi aliyejifunza ambaye anaijua haki, Tawhiyd na shirki kwa ujuzi shubuha za wale wahalifu hazimghuri na wala hazimchanganyi. Bali anaziponda, kufichukua ubatilifu wake na kuwafichulia watu nazo kama mlivosikia katika maneno Yake (Jalla wa ´Alaa):

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا

“Wala hawakujii kwa mfano wowote isipokuwa Tunakuletea haki na tafsiri bora kabisa.”[7]

Mtu wa batili haleti hoja yoyote isipokuwa ndani ya Qur-aan tayari kuna yenye kuivunja na kubainisha upotofu wake. Wao wanatatiza kwa maneno Yake (Jalla wa ´Alaa):

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

 “Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika.”[8]

Hapa kuna hoja gani? Ni kweli kwamba mawalii wa Allaah hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Lakini kuna yeyote amekwambia uwaombe badala ya Allaah? Umebainishiwa ili uwe pamoja nao. Jifunze na unyooke katika kumtii Allaah mpaka uwe pamoja nao. Kitendo cha wao kuwa ni mawalii wa Allaah hakuwafanyi wakafaa kuombwa na kutakwa msaada. Kama ambavyo Mitume ndio waumini bora kabisa na isitoshe ni mawalii wa Allaah. Lakini pamoja na haya haifai kuwaomba badala ya Allaah. Kadhalika waumini wengine waliobaki ni mawalii wa Allaah na ni waja wa Allaah wema. Lakini haifai kwako kuwaabudu kama ambavyo haifai kwako kuwaabudu Mitume. Bali mwabudu Allaah pekee. Amesema (Ta´ala):

فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ

“Basi mwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini.”[9]

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili.”[10]

[1] 25:31

[2] 12:108

[3] 25:33

[4] 37:171-173

[5] 22:40-41

[6] 47:07

[7] 25:33

[8] 10:62

[9] 39:02

[10] 98:05

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 14/10/2021