08. Tafsiri za Qur-aan za Salaf zinazokaribiana

Miongoni mwa maono yanayotokana nao, na ambayo baadhi ya watu wanayazingatia kuwa ni kutofautiana, ni pale wanapoelezea kwa matamshi yanayokaribiana na si kwa maneno yanayoendana sawa.  Kwa sababu sinonimia katika lugha ni chache. Lakini inapokuja katika matamshi ya Qur-aan, ni ima mara chache au hakuna kabisa. Ni mara chache kwamba neno moja linaweza kutafsiri lingine na wakati huohuo kubeba maana yake yote. Badala yake ni kwamba inaleta maana yenye kukaribiana. Hiyo ni sababu moja wapo ya miujiza ya Qur-aan. Pengine mtu akauliza juu ya Aayah isemayo:

يَوْمَ تَمُورُ السَّمَاءُ مَوْرًا

”Siku zitakapotetemeka mbingu kikweli.”[1]

Tukisema kwamba neno (المور) linamaanisha kutikisika, ni tafsiri inayokaribia. Kwa sababu (المور) ni kutikisika kwepesi na kwa haraka. Vivyo hivyo ikiwa mtu atasema kwamba ufunuo (الوحي) kwamba maana yake ni khabari (الإعلام), kwamba Aayah isemayo:

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ

“Hakika Tumekufunulia wahy… ”[2]

maana yake ni kwamba Tumekuteremshia au kwamba Aayah isemayo:

وَقَضَيْنَا إِلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ فِي الْكِتَابِ

”Tuliwafahamisha wana wa israaiyl ndani ya Kitabu… ”[3]

kwamba maana yake Tuliwafunza. Tafsiri zote hizi ni za takriban na si kwa uhakika. Kwani wahy ni khabari ya haraka na iliyojificha, na kuwafahamisha ni maalum zaidi kuliko kuwafunza; kwa sababu ndani yake kuna kuwatumia na kuwafunulia. Waarabu wanaweza kufanya kitenzi kimoja kikusanye maana ya kitenzi kingine, na kitenzi cha pili kikibadilika kama cha kwanza. Kuanzia hapa wako wamekosea wale ambao wamefanya baadhi ya viambishi badala ya vingine, kama wanavyofanya kwa Aayah:

لَقَدْ ظَلَمَكَ بِسُؤَالِ نَعْجَتِكَ إِلَىٰ نِعَاجِهِ

”Hapana shaka amekudhulumu kwa kukuomba kondoo wako kuongezea kondoo wake !”

Kwa maana pamoja na kondoo wako. Vivyo hivyo kuhusiana na Aayah isemayo:

 مَنْ أَنصَارِي إِلَى اللَّـهِ

”Nani watakuwa wasaidizi wangu kwa ajili ya Allaah?”[4]

Kwa maana kwa Allaah. Sahihi ni yale yaliyofanywa na wanasarufi wa Baswrah juu ya ukusanyaji, kwamba takwa lilikuwa linahusiana na kumkusanya kondoo na wa yule mwingine. Vilevile inahusiana na maneno Yake (Ta´ala):

وَإِن كَادُوا لَيَفْتِنُونَكَ عَنِ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ

”Hakika walikaribia kukukengeusha na yale Tuliyokuletea Wahy.”[5]

Kwa maana kukupotosha na kukuzuia. Vilevile inahusiana na maneno Yake (Ta´ala):

وَنَصَرْنَاهُ مِنَ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا

”Tukamnusuru kutokana na watu ambao walikadhibisha Aayah Zetu.”[6]

Inajumuisha maana ya kuwa tulimuokoa na tulimsalimisha. Vilevile inahusiana na maneno Yake (Ta´ala):

عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّـهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا

”Nayo ni chemchem watakayokunywa humo Waja wa Allaah… ”[7]

Inajumuisha maana ya kwamba wanamiminiwa humo. Kuna mifano mingi kama hiyo.

Mwenye kusema kwamba:

لاَ رَيْبَ

”… hapana shaka… ”[8]

kwamba maana yake ni kuwa hapana shaka yoyote ni tafsiri ya kukaribiana. Vinginevyo neno (رَيْب) ndani yake kuna kuchanganyikiwa na mtikiso, kama inavosema Hadiyth:

”Kiache kinachokutia shaka (يريبك)… ”[9]

Hadiyth nyingine inasema kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamuru mtu kumlinda paa aliyepigwa na asimwache yeyote amdhulumu (يريبه)[10]. Kama ambavyo yakini inajumuisha utulivu, basi shaka inakusanya kuchanganyikiwa na mtikiso. Na ingawa shaka inapelekea maana hiyohiyo, tamko lake halifahamishi maana hiyohiyo. Vivyo hivyo inaposemwa kuwa Aayah isemayo:

ذَٰلِكَ الْكِتَابُ

”Hiki ni Kitabu… ”[11]

kunakusudiwa Qur-aan. Ingawa kilichoashiriwa kinaweza kuwa kitu kimoja, ishara iliyotolewa kwa namna ya uwepo wa karibu ni tofauti na ile inayotolewa kwa namna ya kuwa mbali au kutokuwepo. Neno Kitabu linajumuisha maana ya kuwa kimeandikwa na kilicho na maudhui maalum, ambayo hayajumuishwi moja kwa moja katika neno Qur-aan, linaloashiria kile kilichosomwa na kilicho wazi kinachoonekana. Hivyo basi, tofauti hizi zipo ndani ya Qur-aan.

Akisema mmoja wao kwamba Aayah:

أَن تُبْسَلَ نَفْسٌ

”… isije kila nafsi ikaangamizwa…”[12]

kwamba maana yake ni kufungwa na mwingine akasema kwamba ni kuwekwa rehani, basi katika tafsiri zinazopingana ijapo kilichofungwa kinaweza kuwa rehaniwa au kisiwe. Kwa sababu haya, kama tulivotangulia kusema, ni kuleta maana iliyo karibu.

[1] 52:09

[2] 4:163

[3] 17:4

[4] 3:52

[5] 17:73

[6] 21:77

[7] 76:6

[8] 2:2

[9] at-Tirmidhiy (2518). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh at-Tirmidhiy” (2518).

[10] an-Nasaa’iy (2817). Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh an-Nasaa’iy” (2817).

[11] 2:2

[12] 6:70

  • Muhusika: Shaykh-ul-Islaam Ahmad bin Taymiyyah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Muqaddimah fiy Usuwl-it-Tafsiyr, uk. 42-45
  • Imechapishwa: 31/03/2025