02. Kisimamo cha Ramadhaan kina idadi ya Rak´ah maalum

Swali 2: Kisimamo cha Ramadhaan kina idadi ya Rak´ah maalum?

Jibu: Kisimamo cha Ramadhaan hakina idadi maalum kwa njia ya ulazima. Hakuna neno ikiwa mtu atakesha kwa kusimama usiku mzima. Lakini hata hivyo idadi bora ni ile ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiifanya; nayo ni Rak´ah kumi na moja au kumi na tatu. Mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliulizwa ni namna gani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali katika Ramadhaan ambapo akajibu:

”Alikuwa hazidishi katika Ramadhaan wala [mwezi] mwingine zaidi ya Rak´ah kumi na moja.”[1]

Lakini Rak´ah hizi zinapaswa ziwe kwa njia inayokubalika katika Shari´ah. Pia kisomo chake, Rukuu´, Sujuud, kuinuka baada ya Rukuu´ na kitako kati ya sijda mbili zinatakiwa kurefushwa. Haya ni tofauti na yale yanayofanywa na baadhi ya watu hii leo. Wanaziswali kwa haraka inayowazuia waswaliji kufanya kile kinachowapasa kufanya. Uimamu ni usimamizi. Msimamizi anatakiwa kufanya kile ambacho kina manufaa na manufaa zaidi. Kule imamu kutilia umuhimu tu wa kumaliza mapema ni kosa. Bali kinachompasa ni yeye kufanya kile kilichokuwa kinafanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kurefusha usimamaji, Rukuu´, Sujuud na ukaaji kitako kutegemea na yale yaliyopokelewa. Aidha akithirishe du´aa, kisomo, Tasbiyh na mengineyo.

[1] al-Bukhaari7 (1147-3569) na Muslim (1670).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 8-10
  • Imechapishwa: 10/04/2021