Zakaat-ul-Fitwr ni wajibu kwa muislamu ambaye ana chakula cha mchana na usiku


Swali: Ni ipi hukumu ya swadaqah ya Fitwr? Je, imelazimishwa ipitikiwe na mwaka mzima? Je, aina zinazotolewa zimefanyiwa kikomo? Mambo yakiwa ni hivyo ni zipi? Je, mtu analazimika kuwatolea watu wa nyumbani kwake akiwemo mke na mfanya kazi?

Jibu: Zakaat-ul-Fitwr imefaradhishwa kwa kila muislamu, mdogo kwa mkubwa, mvulana kwa msichana, muungwana na mtumwa. Imethibiti kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifaradhisha Zakaat-ul-Fitwr pishi ya tende au pishi ya shayiri ni lazima kwa mvulana, msichana, mdogo, mkubwa, muungwana na mtumwa wa Kiislamu. Aliamrishwa itolewe kabla watu hawajatoka kuswali.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Haina utaratibu wa kusubiri itimize mwaka. Bali ni wajibu kwa muislamu kujitolea mwenyewe, watu wa nyumbani kwake wakiwemo watoto, wakeze na wale anaowamiliki ikiwa yuko na chakula cha kuweza kuwakimu mchana na usiku wake.

Kuhusu mfanya kazi ambaye ameajiriwa mwenyewe anatakiwa ajitolee zakaah. Isipokuwa ikiwa kama alimuwekea sharti [kabla ya kuanza kazi].

Kuhusu yule mfanya kazi ambaye ni mmilikiwa zakaah yake inamlazimu yule bwana wake, kama ilivyotangulia katika Hadiyth.

Ni wajibu kutoa katika kile chakula kinacholiwa katika mji. Ni mamoja ikawa tende, shayiri, mchele, mahindi na vinginevyo. Hayo ndio maoni sahihi zaidi ya wanachuoni. Kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakushurutisha katika hilo aina maalum. Ni jambo lenye wasaa.

[1] al-Bukhaariy (1503).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (14/197-198)
  • Imechapishwa: 12/06/2018