36Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali.” 37Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko. 38Hapo akawaambia: “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.” 39Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe.” 40Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro: “Ndio kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho inataka lakini mwili ni dhaifu.” 42Akaenda tena mara ya pili akasali: “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kipite bila mimi kukinywa, basi, utakalo lifanyike.” 43Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi. 44Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale. 45Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia: “Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi. 46Amkeni; twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti.”

  • Marejeo: Mathayo 26:36
  • Imechapishwa: 03/02/2020