Swali: Tunaona baadhi ya waswaliji wamerefusha kucha zao na zimefunikwa na uchafu. Je, kitendo hichi kinaafikiana na dini? Je, wudhuu´ unasihi?

Jibu: Kucha ni lazima kuyapatiliza kabla ya kuzidi nyusiku arobaini. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwawekea watu muda wa kukata kucha, kunyoa nywele za sehemu ya siri, kunyofoa nywele za kwapani na kupungusa masharubu mtu asiache zaidi ya nyusiku arobaini. Hivi ndivo imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yamesemwa na Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye alikuwa mfanyi kazi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Alituwekea muda kupunguza masharubu, kukata kucha, kunyofoa nywele za kwapani na kunyoa nywele za sehemu ya siri kwamba tusiache chochote katika hivyo zaidi ya nyusiku arobaini.”

Ameipokea Imaam Muslim katika “as-Swahiyh” yake. Pia ameipokea Imaam Ahmad, an-Nasaa´iy na Jamaa´ah kwa tamko lisemalo:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituwekea muda tusiache kucha, masharubu, kunyoa nywele za sehemu ya siri na kunyofoa nywele za kwapani zaidi ya nyusiku arobaini.”

Kwa hivyo ni lazima kwa wanawake na wanamme kuzingatia jambo hili. Wasiache kucha, masharubu na nywele za sehemu ya siri wala nywele za kwapani zaidi ya nyusiku arobaini.

Wudhuu´ ni sahihi na haubatiliki kutokana na ule uchafu unaoweza kupatikana chini ya kucha. Kwa sababu ni uchafu mdogo wenye kusamehewa.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/50)
  • Imechapishwa: 07/08/2021