Wazazi wa Mtume wako Motoni


2592- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Baba yangu na baba yako wako Motoni.”

Ameipokea at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (3552): Muhammad bin ´Abdillaah al-Hadhwramiy ametuhadithia: Abu Kurayb ametuhadithia: Abu Khaalid al-Ahmar ametuhadithia, kutoka kwa Daawuud bin Abiy Hind, kutoka kwa al-´Abbaas bin ´Abdir-Rahmaan, kutoka kwa ´Imraan bin al-Huswayn ambaye amesema:

”Huswayn alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Unasemaje juu ya mtu ambaye alikuwa akiunga udugu na akiwakirimu wageni lakini akafa kabla yako?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Baba yangu na baba yako wako Motoni.”

Mimi wakati niko nayaandika haya natambua kuwa baadhi ya wale wanaozikataa Hadiyth hizi wanazipindisha maana ambayo ni batili. Kwa mfano hayo yamefanywa na as-Suyuutwiy – Allaah atusamehe sisi na yeye – katika baadhi ya vijitabu vyake. Kilichowapelekea kufanya hivo ni kuchupa kwao mipaka katika kumtukuza na kumpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Matokeo yake wanapinga yale aliyoeleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba wazazi wake walikuwa makafiri. Ni kama kwamba wao wana huruma zaidi juu yao kumshinda yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu ya kutojichunga wako ambao wanataja Hadiyth iliotangaa inayosema kwamba Allaah alimuhuisha mama yake na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwamini. Upokezi mwingine unataja wazazi wote wawili. Hadiyth hiyo imezuliwa na ni batili kwa mujibu wa wanachuoni kama vile ad-Daaraqutwniy, al-Juurqaaniy, Ibn ´Asaakir, adh-Dhahabiy na al-´Asqalaaniy. Ibn-ul-Jawziy amesema:

”Hapana shaka yoyote kwamba Hadiyth hii imezuliwa. Walioizua ni watu wenye uelewa mchache na elimu ndogo. Vinginevyo angelikuwa na elimu basi angelitambua kuwa ambaye amekufa kwenye ukafiri basi haimnufaishi kitu kuamini baada ya kufufuliwa. Maneno Yake (Ta´ala) yanatosha katika kuraddi Hadiyth hii:

 وَمَن يَرْتَدِدْ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ فَأُولَـٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Atakayeritadi miongoni mwenu kutoka dini yake ambapo akafariki hali ya kuwa ni kafiri, basi hao yameporomoka matendo yao duniani na Aakhirah na hao ni watu wa Motoni wao humo watadumu.”[1]

Vilevile maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Nilimtaka idhini Allaah kumuombea msamaha mamangu ambapo hakunipa idhini. Nikamuomba idhini kulitembelea kaburi lake akanipa idhini.”[2][3]

[1] 02:217

[2] Muslim (976).

[3] al-Mawdhwuu´aat (1/284).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (6/1/181)
  • Imechapishwa: 27/04/2019